Rais Magufuli amewatangazia kiama wauaji wa tembo ndani na nje ya nchi na kumtaka Mkuu wa Hifadhi ya Selous kujipanga vizuri.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana, wakati akizindua barabara ya kilomita 193 ya Namtumbo, Kilimasera, Matemanga hadi Tunduru, katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
“Washtakiwa wa eneo hili wengi ni wanaoua tembo, unakuta Watanzania wanashirikiana na majangili wa nchi jirani, wakiua tembo huku wanawapeleka kule na wakiua tembo kule wanawaleta huku.
“Mtandao wote tumeshaujua, mkae mwendo wa mchakamchaka, wapo wengine wanashirikiana na viongozi, ninafahamu circle.
“Tunataka Selous iwepo, sasa anayehusika na Hifadhi ya Selous ajipange vizuri, wengine wanaoshirikiana na kutengeneza mtandao ni watendaji kazi wa Selous,” alisema.
Akizungumzia barabara hiyo, Rais Magufuli alisema ujenzi wa kilomita 193 si kazi ndogo na umetumia zaidi ya Sh bilioni 173.3.