Redio ya Magic FM na Free Afrika zimeonywa na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kitendo cha kusoma habari za magazeti kwa undani kinyume cha agizo la serikali.
Akisoma uamuzi wa Kamati hiyo baada ya kupitia maelezo ya utetezi kwa redio hizo mbili, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Valerie Msoka, alisema agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, limezuia kusoma habari kwa undani na badala yake inatakiwa kusomwa vichwa vya habari vya magazeti.
Alisema Kamati iliandika wito kwa uongozi wa Magic FM kuwataka kuwasilisha utetezi wao wa maandishi ni kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kukiuka agizo la waziri.
"Katika kipindi chake cha Morning Magic tulikisikiliza kipindi walichokuwa wanapitia magazeti ili kujiridhisha walisoma habari za magazeti kwa undani kinyume cha agizo la serikali," alisema Msoka.
Msoka alisema katika maelezo yao Magic FM ilidai kuwa kosa hilo lilifanywa na uongozi uliopita,
Aliendelea kueleza kuwa ni kweli kipindi kilikiuka agizo la serikali na kwamba uongozi huo mpya hauna rekodi ya kupatiwa barua ya kukiuka agizo la serikali.
Alisema waliomba radhi na kudai kuwa kosa hilo halitajitokeza tena katika uongozi huu mpya watazingatia agizo la serikali.
Aidha, Msoka alisema Kamati yake imebaini kuwa walifanya kosa hilo kwa makusudi na utetezi wao hauna msingi na kwamba kubadilika kwa uongozi siyo sababu ya kuvunja agizo la serikali.
Alisema hata kama uongozi umebadilika wafanyakazi wa Magic ni wale wale, hivyo walitakiwa kuzingatia maagizo yaliyotolewa.