Serikali imenunua mtambo mkubwa wa madini ambao utasaidia kufanya utafiti wa madini, sambamba na kuwasaidia wachimbaji wadogo katika shughuli za madini nchini
Akizungumza Bungeni leo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema kuwa Serikali imefikia uamuzi huo kwa lengo kuunga mkono wachimbaji wadogo nchini kote wakiwemo wachimbaji wa kijiji cha Busiri wilaya ya Biharamulo.
Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa ili kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini, Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imenunua mtambo mkubwa wa kumsaidia kufanya utafiti wa kina kwa kuchoronga miamba kwa bei nafuu ili kubaini mashapo zaidi na kuongeza uzalishaji.
Naibu Waziri, Nyongo aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa wachimbaji wadogo ili wanufaike zaidi na kazi ya uchimbaji.
Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini inakamilisha uandaaji wa kitabu cha madini yapatikanayo Tanzania toleo la nne ambacho kitaonesha uwepo wa madini katika mikoa, wilaya na vijiji, ambapo kitasaidia wachimbaji wadogo kutambua madini yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na matumizi ya madini hayo.
Aidha, Wizara kupitia Mradi wa Usimamizi endelevu wa Raslimali Madini (SMMRP), inakamilisha kujenga vituo vya umahiri katika wilaya ya Bukoba, Bariadi, Songea, Handeni, Musoma, Mpanda na Chunya ili kuwezesha wachimbaji wadogo kujifunza kwa vitendo.