Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas amekiri kuwa ni kweli vyombo mbalimbali vya habari vilivyoripoti uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) uliofanywa na Mbunge Zitto Kabwe vimeandikiwa barua.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter Dk. Abbas ameandika akimuonya kiongozi huyo wa Chama cha ACT Wazalendo kuacha kile alichokiita ni upotoshaji, na kuleta siasa katika taaluma ambayo haielewi.
Awali Zitto Kabwe aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa magazeti yote yaliyoandika uchambuzi huo yaliandikiwa barua na kutakiwa kujieleza kwa kukiuka sheria
"Msemaji Mkuu kaandikia barua magazeti yote yaliyoandika habari ya uchambuzi wa Ripoti ya CAG uliofanywa na @ACTwazalendo. Amewataka wajieleze kwa kuvunja sheria. Sasa Msemaji wa Serikali amekuwa Mhariri Mkuu wa Taifa. Vyombo vya Habari vinatishwa kuandika Habari kutoka upinzani "
Katika maelezo yake Dkt Abbas amemtaka mbunge huyo kutoleta siasa kwenye taaluma asiyoielewa na kwamba walioandikiwa barua wameelewa na/au wamekiri kosa.
"Usilete siasa katika taaluma ambayo bahati mbaya huijui misingi yake. Walioandikiwa wamejua/kukiri kosa lao."
Hata hivyo msemaji huyo hakuweka wazi kuwa ni kosa gari vyombo hivyo hivyo vimekiri au wameomba msamaha kwa kosa gani.
Lakini aliendelea kusema kwamba, kama vyombo hivyo vimeandikiwa barua kisha vikaenda kuripoti kwake (Zitto), basi hilo linadhihirisha kuwa yeye ndiye amekuwa akivipotosha kila mara.
"Kama waliandikiwa, wakaripoti kwako sasa tumejua wewe ndie Mhariri Mkuu unaewapotosha kila siku. Acha. "