Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kitendo cha Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa Assad kuendelea kuwepo ofisini mpaka sasa ni kumpa rais wakati mgumu kwa kuwa wao bunge wameshaeleza kuwa hawamtaki
Ndugai ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanahabaji Jijini Dodoma ambapo amesema kwamba kwa kitendo cha Bunge kumkataa Prof Assad alipaswa ajiongeze kwa kujiuzulu.
"Tunataka tumuoneshe Prof. Assad kuwa Bunge halichezewi, simuelekezi kazi ila anatakiwa ajiongeze kama ni kujiuzulu au la! maana tushamwambia hatumtaki, anavyoendelea kubaki ofisini ni kumpa tu wakati mgumu Rais.
"Sisi kama Bunge hatutaki hilo neno dhaifu, kwa sababu Bunge kama Bunge halifanyiwi tathmini na ofisi ya CAG ila wanaofanyiwa tathmini ni watendaji wa Ofisi hiyo hivyo hawakupaswa kudhihakiwa na lugha hiyo inayotajwa kuwa ya kihasibu".
Aidha kuonyeshwa kukerwa na neno 'Dhaifu analoendelea kulitumia Prof Assad, Ndugai amesema kwamba kama yeye analipenda sana neno hilo ajiite na kwamba wao kama bunge wameikataa na hawalipendi.
Kuhusu kazi za CAG, Spika amefafanua kwamba; "Hatuna tatizo na ripoti ya CAG…tatizo letu ni maneno ambayo Prof. Assad ameyatoa akiwa Marekani, na alipoita waandishi akarudia tena, maneno yale sie tumeyakataa sio ya kistaarabu.
Spika Ndugai amemsifu Profesa Assad kwa ujasiri wake huku akiufananisha na ujasiri wa mbwa kumtukana mtu anayemlisha.
"Unatukana hadi mkono unaokulisha, inahitaji ujasiri na jamaa ana ujasiri. Ila ni ujasiri ule wa mbwa anayemtukana anayemlisha," amesema.
Hata hivyo, Ndugai amesema hana chuki binafsi na Assad bali tatizo ni lugha tu aliyotumia ya kuliita Bunge dhaifu.