Umoja wa Mataifa walaani matumizi ya silaha nzito Libya

Mjumbe msaidizi wa Umoja wa Mataifa Libya umelaani ongezeko la matumizi ya silaha nzito na mashambulizi holela dhidi ya makazi ya watu, shule na miundombinu na kutaka huduma za dharura kuwafikia raia waliokwama

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, idadi ya watu wasio na makazi ndani na nje ya mji wa Tripoli hivi sasa inakaribia 20,000. Zaidi ya watu 2,400 walikimbia makazi yao katika kipindi cha masaa 24 pekee.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujaric, amewaambia waandishi wa habari jijini New York kwamba familia nyingi zinazokimbia maeneo yaliyo na machafuko zinaelekea katikati mwa Tripoli na maeneo ya karibu, lakini takribani watu 14,000 wasio na makazi wametafuta hifadhi nje ya mji huo mkuu katika maeneo ya Tajoura, Al Maya, Ain Zara na Tarhouna.

"Mjumbe maalum wa katibu mkuu anafanya kazi na serikali na pande zote Libya, sambamba na wawakilishi wa kimataifa kujaribu kusitisha mapigano, na kusonga mbele na mchakato wa kisiasa. Ninafikiri Bw. Salame alikuwa wazi kwamba mkutano wa kitaifa haukufutwa. Anataka kuendelea nao lakini hilo halitawezekana ikiwa watu wanafyatuliana risasi na kuwaua raia, alisema Dujaric.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilianza kujadili azimio lililoandaliwa na Uingereza la kutaka kusitishwa mapigano nchini Libya, baada ya majeshi tiifu ya kamanda Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi mjini Tripoli.

Azimio hilo linaonya kuwa mashambulizi ya jeshi la Haftar yanatishia usalama na mustakabali wa mazungumzo ya kisiasa yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa, sambamba na upatikanaji wa suluhisho la kisiasa la mgogoro huo. Baraza hilo pia limezitolea wito pande zote zinazohusika nchini Libya, kuheshimu usitishaji mapigano na kushiriki katika mazungumzo ya kuhakikisha hali ya usalama inarejea kote nchini Libya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad