Upinzani Wamtaka Spika Ndugai Ajiuzulu

Upinzani Wamtaka Spika Ndugai Ajiuzulu
Muungano wa vyama nane vya upinzani nchini Tanzania umemtaka Spika wa Bunge la nchi hiyo Job Ndugai kujiuzulu wadhfa wake.

Tamko hilo la upinzani linatokana na mvutano mkali unaoendelea baina ya Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa nchi hiyo Prof Mussa Assad.

Jana Jumapili, Spika Ndugai aliwaambia bwana Assad anafaa kujitathmini na kuchukua uamuzi wa kujiuzulu baada ya Bunge kuazimia kutofanya kazi naye.

Ndugai pia alidai Assad "anampatia wakati mgumu" rais John Magufuli, na kumtaka aende mbele yake (rais) kujieleza.

Kauli hizo za Spika zimepingwa vikali na muungano huo wa upinzani unaoundwa na vyama vya Chadema, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, NLD, DP, UPDP, CHAUMMA na CCK.

Vyama hivyo vinadai kuwa kama kuna anayetakiwa kijiuzulu kwenye sakata hilo ni Spika Ndugai na si CAG Assad.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Mwenyekiti wa UPDP, Bwana Fahmi Dovutwa amedai taifa (Tanzania) inaingizwa kwenye mgogoro usio wa lazima.

"Kutangaza kwamba CAG akitaka aende akamuombe radhi Raisi. Hili nalo ni mkanganyiko. Sasa (Spika Ndugai) anataka kuingiza mgogoro baina ya ofisi ya raisi na bunge. Ni mgogoro ambao hauna ulazima. Labda atuambie yeye Spika anataka Raisi afanye nini... kitendo cha spika kugonganisha bunge na raisi ni kushindwa kazi na ajiuzulu," amesema Dovutwa na kuongeza "Tumtake tu CAG aendelee kusimama na msimamo wake, wananchi na upinzani tupo nyuma yake. Spika yeye kama kuna lililomkera basi akereke kwa kushuka kwenye jukwaa la Uspika Bungeni."



Dovutwa amesisitiza kuwa kwa hatua ambayo suala hilo limefikia, Bunge linapaswa kupokea na kuzingatia hoja za wananchi. "Huko nyuma, misingi ya Taifa letu tulioachiwa na Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) ni kuwa viongozi wakubali kukosolewa, wasiwe wakali na wasichukie wanapokosolewa. Hatari iliyokuwepo ya msimamo wa Spika akiwa na kesi mahakamani anaweza kumkataa Jaji Mkuu."

Naye kiungozi wa muungano huo wa upinzani na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amesema kauli za jana za Spika ni kinyume cha azimio lilipitishwa bungeni. "Haya mengine wala si ya Azimio la Bunge, ni yake Spika mwenyewe."

Takribani wiki mbili zilizopita, Bunge liliazimia kutofanya kazi na CAG baada ya 'kumkuta na tuhuma' za kulidharau Bunge.

CAG alifanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Disemba 2018 ambapo alisema kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad