Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa(EACC), leo asubuhi imewakamata wakiwa nyumbani kwao, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Ardhi(NLC), Muhammad Swazuri na Maafisa wengine wa Tume hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Waliokamatwa watashtakiwa kwa makosa mengi yakiwemo Matumizi mabaya ya ofisi, kula njama ya kutaka kufanya makosa ya kiuchumi na utakatishaji fedha.
Kukamatwa kwao kunahusishwa na ulipaji fidia usio wa halali kwenye ardhi iliyochukuliwa na Tume ya Ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Standard Gauge Railway(SGR) ambapo mwaka 2013 Mamlaka ya Barabara iliitaka Tume hiyo kutafuta ardhi.
Tume ilipata ardhi iliyokuwa ikimilikiwa na M/s Tornado Carriers Ltd iliyokadiriwa kuwa na thamani ya Ksh. 34,501, 110 kwa mwaka 2015, Tume ilipotaka kulipa fedha hizo ili kununua ardhi hiyo Tornado Carriers ilikataa kuuza na hivyo Tume ikaamua kufanya makadirio mapya ya thamani
Yalipofanywa makadirio kwa mara ya pili, ardhi ile ilikuwa na thamani ya KSh 109,769,363 kwa mwaka 2017, Mamlaka ya barabara ililipa KSh 55,269,363 kwa M/s Tornado Carriers Ltd na 54,500,000 kwa Wanasheria, C.W Chege and Co.
Mwaka 2018, Swazuri, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli, Atanas Maina na watu wengine watano walikamatwa kwa kulipa malipo ya fidia ya kifisadi kwenye ujenzi wa Standard Gauge Railway lakini waliachiwa kwa dhamana.