Vikwazo Vipya Uturuki Endapo Ikinunua Makombora ya S-400 kutoka Russia

Vikwazo Vipya Uturuki Endapo Ikinunua Makombora ya S-400 kutoka Russia
Uhusiano wa Marekani na Uturuki umekumbwa na msuguano mkubwa hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli ya Julai 2016. Baada ya Uturuki kusambaratisha mapinduzi hayo, ilisema kuwa Marekani ilihusika katika njama hiyo na kwa msingi huo uhusiano wa nchi hizo mbili uliingia baridi.

Kinyume na matumaini ya wakuu wa Uturuki kuhusu kuboreka uhusiano wa pande mbili katika urais wa Donald Trump, hitilafu za nchi hizo mbili zinaonekana kushadidi.

Moja ya nukta muhimu za hitilafu baina ya Marekani na Uturuki ni sisitizo la wakuu wa Ankara kuhusu kununua mfumo wa makombora ya kujihami angani ya S-400 kutoka Russia.

Disemba 2017, Uturuki na Russia zilitiliana saini mapatano ya kununua mfumo huo wa S-400 na punde baada ya hapo Marekani ilianza kuwashinikiza wakuu wa Ankara wabatilishe mkataba huo. Hatua ya Uturuki ya kununua silaha hiyo muhimu ya Russia si tu kuwa ilipingwa vikali na Bunge la Marekani, Congress, na wizara ya ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon, bali pia Washington imesonga mbele na kuchukua hatua za kivitendo kuizuia Uturuki kununu mfumo huo wa kujihami.

Uturuki ni mwanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Atlantiki ya Kaskaizni (NATO)  ambao unaongozwa na Marekani na unaoitazama Russia kama hasimu wake mkuu.

Kwa msingi huo Marekani imedai kuwa kuingiza mfumo wa S-400  katika mtandao wa kujihami angani wa nchi ya NATO ni jambo ambalo litapelekea Russia igundue siri za udhaifu wa ndege za kivita za nchi wanachama wa NATO hasa udhaifu wa ndege ya kivita ya Marekani ya kizazi cha tano ya F-35.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad