Maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Algeria, Algiers, wakiipinga serikali ya mpito. Maandamano hayo ya jana yalifanyika pia kwenye miji ya Oran, Constantine na Annaba, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Hayo yalikuwa maandamano ya wiki ya tisa na ya kwanza tangu Tayeb Belaiz kujiuzulu kama mkuu wa Baraza la Katiba hapo Jumanne.
Baraza hilo ndilo lililopewa jukumu la kusimamia uchaguzi. Waandamanaji wanataka pia rais wa mpito, Abdelkader Bensalah, na waziri mkuu wake, Noureddine Bedoui, kuachia madaraka.
Wote watatu ni watu wa karibu sana na serikali ya rais wa zamani, Abdelaziz Bouteflika, ambaye alijiuzulu mapema mwezi huu baada ya miaka 20 kuwepo madarakani.
Siku ya Jumanne, mkuu wa jeshi aliwaomba wananchi kuwa na subira kwenye kipindi cha mpito, huku uchaguzi wa rais ukipangwa kufanyika tarehe 4 Julai, ili kumchaguwa mrithi wa Bouteflika.