Uongozi wa Soko kuu la majengo Jiji la Dodoma limeanza kufanya uhakiki wa wabeba mizigo na waendesha mikokoteni zaidi ya 214, ili kuwapatia vitambulisho na sare vitakavyo wawezesha kutambuliwa kwa uongozi na wateja.
Uhakiki huo wa kuwapatia vitambulisho hivyo ambao kwa pamoja unafanywa na uongozi wa soko, kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wafanyabiashara umetokana na baadhi ya wabeba mizigo na waendesha mikokoteni kuletewa malalamiko ya kushiriki katika vitendo vya wizi kwa wateja.
Katibu mkuu wa soko hilo, Eliamani Mollel alisema kuwa kutolewa kwa vitambulisho hivyo pia itasaidia kuwatambua wabeba mizigo ili kurudisha imani kwa wateja wanaopata huduma na wale wanaoleta mizigo ya jumla.
Alisema kuwa hivi sasa soko hilo limekuwa na kundi kubwa la vijana ambao wanafanya kazi ya kubeba mizigo, lakini hata hivyo kuna baadhi yao siyo waaminifu kwenye mizigo ya wateja.
“Kutokana na vijana hao baadhi yao kutokuwa na uaminifu, sisi kama viongozi tumepata malalamiko kutoka kwa wateja mbalimbali wanaopata huduma mbalimbali za bidhaa, na moja ya malalamiko hayo ni kuibiwa kwa mizigo” alisema.
Aidha katibu huyo alitoa tahadhali kwa wateja wanaopata huduma mbalimbali kuwatumia wabeba mizigo na wasukuma mikokoteni wenye vitambulisho na waliovaa sare ili kuepukana na udanganyifu unaoweza kutokea.
Kwa upande wao wabeba mizigo na wasukuma mikokoteni pia wameshauriwa kuvaa vitambulisho na sare kwenye maeneo yao ya kazi ili waweze kutambuliwa pindi wanapohitajika kutoa uhuduma ya ubebaji wa mizigo.