Watu wanne ambao ni waganga wa jadi maarufu kama Rambaramba wanashikiliwa na jeshi la Polisi Wailayani Tabora mkoani Tabora kwa kuweka mazindiko katika Shule ya msingi Ndevelwa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Tabora Emmanuel Nley amesema watu hao walikuwa wanafanya mazindiko katika Shule hiyo ambapo wanafunzi walikuwa wanaanguka darasani.
“Hawa waganga maarufu kama kamchape au lambalamba wanafanya lamli na kuwaaminisha wananchi imani za kishirikina na kusababisha mauaji na migogoro katika jamii”, Amesema Nley.
Kamanda Nley amesema wameweza kuwakamata viongozi wa kijiji akiwemo Rashidi Ally Mwenyekiti wa kijiji cha Ndevelwa, Emmanuel Jacobo Mwenyekiti wa mtaa, Ramadhani Juma Mwenyekiti kamati ya wazazi Shule ya msingi Ndevelwa.
“Hawa viongozi wa kijiji walikubaliana kuwaita na kuwahifadhi waganga hawa ili kuzuia mapepo yaliyokuwa yanawaangusha wanafunzi darasani mbapo ni kinyume cha sheria”amesema Nley
Aidha amewataka wananchi mkoani humo kuachana na mila potofu na kuwaamini waganga wa jadi kwani ndio chanzo cha migogoro na kusababisha mauaji katika jamii.