Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini Mkoani Shinyanga kumpisha mwekezaji ambaye ni mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu wa kampuni ya Hanan Afro Asia Geo Engineering (T) Limited kutoka China kuendelea na maandalizi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu, kwa kuwa ndiye aliyewekeza katika kijiji husika kwa kufuata sheria na kanuni zake.
Naibu Waziri Nyongo ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 03 Aprili, 2019 katika mkutano wake wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa wa Shinyanga yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jasinta Mboneko, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Kamando, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba, Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa, wataalam kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na waandishi wa habari.
Alisema kuwa, kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo na mwekezaji kutoka nchini China ambaye ni kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited ambapo malalamiko yaliwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli katika ziara yake aliyoifanya Wilayani Kahama Machi 10, 2018 ambapo alielezwa kuhusu unyanyasaji uliofanywa wakati wa zoezi la uthamini na ulipaji wa fidia kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kupisha uanzishwaji wa mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu.
Aliendelea kusema kuwa katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli Machi 11, 2018 aliyekuwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alitembelea eneo la Mwakitolyo linalolalamikiwa kwa lengo la kufanya mkutano na kusikiliza malalamiko ya wananchi ambapo baada ya kusikiliza malalamiko hayo aliahidi kwenda kufanyia kazi malalamiko yao na kuwapa mrejesho.
Aliendelea kueleza kuwa, iliundwa timu maalum kwa ajili ya kufanya uchunguzi kulingana na hadidu rejea iliyokuwa imepewa ambayo iliitaka timu kukutana na viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya, kuainisha majina ya wananchi waliolipwa na ambao hawajalipwa fidia, vigezo vilivyotumika wakati wa uthaminishaji na ulipaji wa fidia pamoja na mapendekezo mbalimbali.
Nyongo aliendelea kufafanua kuwa, mara baada ya timu kumaliza kazi yake, ilibainika kuwa mwekezaji alilipa kiasi cha shilingi bilioni 1.63 kama fidia kwa wananchi waliokuwa katika eneo husika hivyo zoezi kukamilika kwa asilimia 99.6.
Alisisitiza kuwa pamoja na wananchi takribani 375 kulipwa fidia bado ilionekana kuwa wananchi wengi waliolipwa fidia sio wanakijiji wa Mwakitolyo na kuongeza kuwa wananchi 40 tu ndio walioonekana wamiliki halali wa mashamba pamoja na makazi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo aliitaka Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kuharakisha upatikanaji wa maeneo mapya kwa ajili ya wanananchi 40 ambao ni wamiliki halali wa makazi na mashamba katika kijiji cha Mwakitolyo ili mwekezaji aweze kuanza shughuli za uchimbaji mara moja.
Aidha, Naibu Waziri Nyongo alimtaka Mkurugenzi wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited kuhakikisha anadumisha mahusiano na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo na kumtaka kuhakikisha anashiriki katika uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu, barabara kama Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake inavyofafanua.
Wakati huo huo Nyongo aliwataka wananchi kumpa ushirikiano mwekezaji ili kufaidi matunda ya uwekezaji kwenye kijiji chao ikiwa ni pamoja na ajira kwa wazawa, utoaji wa huduma za vyakula, biashara, huduma za jamii hivyo kupaisha uchumi wa kijiji hicho.
Aliendelea kusema kuwa, madini ni mali ya watanzania wote, hivyo baada ya uwekezaji kuanza kampuni hiyo italipa kodi mbalimbali kwenye halmashauri na Serikali kuu hivyo kuboresha sekta nyingine kama vile miundombinu, afya, elimu n.k.
Naye Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum akizungumza katika mkutano huo mbali na kumpongeza Naibu Waziri Nyongo kwa kutatua mgogoro huo, aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii huku wakilinda amani ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited, Zhang Jiangho mbali na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu, aliahidi kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kwa kuboresha huduma za jamii na kulipa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.
Wananchi Watakiwa Kumpisha Mwekezaji Kuchimba Dhahabu
0
April 05, 2019
Tags