Watawa wawili wa kiume wa Kanisa la Khufti (Coptic) wamehukumiwa kifo nchini Misri kwa mauaji ya askofu mwaka 2018, maafisa wa Cairo wamethibitisha.
Askofu Epiphanius, 64, alipatikana akiwa ameuawa na kuvuja damu nyingi ndani ya makazi ya kanisa kaskazini magharibi mwa jiji la Cairo mwezi Julai 2018.
Mamlaka za Misri zilihusisha tukio hilo na ugomvi ambao haukuwekwa wazi baina ya watawa hao na askofu Epiphanius.
MATANGAZO
Hukumu ya kunyongwa ilipitishwa mwezi Februari mwaka huu na kisha kupelekwa kwa mufti mkuu wa Misri ili kupitishwa.
Mmoja wa watawa hao, Wael Saad, anaripotiwa kukiri mbele ya waendesha mashtaka kuwa alitumia nondo kumshambulia askofu huyo mpaka kufikwa na umauti.
Mtawa mwengine, Remon Rasmi, alishtakiwa kwa kosa la kumpatia Saad usaidizi.
Saad and Rasmi, ambao pia walikuwa wakifahamika kwa majina yao ya kikanisa ya Ashiah na Faltaous, wanaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Kiongozi wa Kanisa la Khufti Papa Tawadros II amechukua hatua kadhaa kurejesha nidhamu
Kesi hiyo imewaacha wengi ndani ya kanisa la Khufti na bumbuwazi.
Wafuasi wa kanisa hilo wanafikia asilimia 10 ya raia wote wa Misri.
Baada ya mauaji hayo, kiongozi wa kanisa hilo, Papa Tawadros II, alitangaza hatua mbali mbali zilizolenga kurejesha nidhamu baina ya watumishi wa kanisa.
Mosi amesitisha uandikishaji wa watawa wapya kwa kipindi cha mwaka mzima, na pili watawa wote wametakiwa kufunga kurasa zao zote za mitandao ya kijamii.
Wakhufti walijitenga na madhehebu mengine ya kikristo mwaka 451, hivyo ni moja ya makanisa makongwe zaidi duniani.
Kanisa hilo linachukuliwa kuwa ndio kubwa zaidi katika Mashariki ya Kati, na pia lina wafuasi zaidi ya milioni moja nje ya Misri.
Watawa wawili wa Kanisa la Khufti la Misri wahukumiwa kunyongwa kwa kumuuwa askofu
0
April 26, 2019
Tags