Rundo la pesa bandia za kigeni na vipande vya dhahabu vimekamatwa wakati wa uvamizi uliofanywa katika jengo moja Jijini Nairobi, Kenya.
Maafisa kutoka Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa uhalifu nchini Kenya (DCI) wamesema kuwa wamewatia nguvuni pia washukiwa 8, miongoni mwao wakiwa ni raia wa kigeni.
"Katika uvamizi huo uliofanyika mapema Jumanne asubuhikatika barabara ya Kiboko/Mukoma mamilioni ya dola feki za Marekani yamekamatwa pamoja na pesa za Zambia- Kwacha pamoja na kilo 100 za vipande vya dhahabu feki. Raia wanne wa kigeni: Mkongo 1, Watanzania 2 , Mnaigeria 1 na Wakenya 4 wamekamatwa. Watafikishwa mahakamani ,"Ilisema taarifa ya makao makuu ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI iliyotumwa kwenye ukurasa wa Tweeter.
Wakenya waliokamatwa wametambuliwa kama : Bwana Boniface Mtwasi Anjere, Bwana Robert Riagah, Bwana Arthur Caleb Otieno na Bwana Michael Omondi Okengo.
Raia wa kigeni walikamatwa wametajwa kuwa ni Watanzania Manson Chogga Mtassi na Konie Kalist, Raia wa Kongo- Kinshasa Ruhota Kabagale na Mnaigeria Chukunosho Francis Ogbuanu.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, mabilioni ya fedha gushi yamekamatwa katika maeneo ya jiji la Nairobi.
Mwezi Februari, polisi walisema walikamata pesa bandia sawa na shilingi bilioni 32 katika nyumba moja maeneo ya Ruiru, Kiambu viungaji mwa jiji la Nairobi na mwezi Machi walikamata shilingi bilioni 2 zilizokuwa feki katika tawi la benki ya Barclays zilizokuwa zimewekwa kwenye boksi lililotengwa kwa ajili ya pesa zilizowekwa na wateja: Kenya: Polisi waivamia benki kwa msako wa pesa bandia
Lakini mmiliki wa pesa hizo, Bwana Eric Adede, alikanusha kuwa pesa hizo zilikuwa bandia na akaiomba benki iwaaamuru polisi kuleta pesa hizo mahakamani.