Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema Serikali haipo tayari kufungua mgodi wa dhahabu wa Nyarugusu uliopo kata ya Nyarugusu wilayani Geita hadi pale wamiliki watakapotimiza masharti waliyopewa pamoja na kurudisha dhahabu kilo 5.72 wanazodaiwa kutorosha Oktoba mwaka jana.
Mgodi huo ambao leseni ni yake ni ya Watanzania walioingia ubia na raia wa kigeni ulifungwa na wizara hiyo kwa kosa la kutorosha dhahabu lakini wamiliki wa leseni wanadai kosa hilo lilifanywa na wabia na sio wao.
Akizungumza baada ya kutembelea mgodi huo jana, Biteko alisema baadhi ya Watanzania siyo wema kwa wawekezaji na wanasababisha jina la nchi kuchafuliwa na wawekezaji kuogopa kuwekeza kutokana na ujanja ujanja unaofanywa na wazawa.
Amesema hata fungua mgodi huo hadi pale wamiliki watakaporudisha dhahabu iliyotoroshwa, kumaliza migogoro wa wao kwa wao kati ya wenye hisa na wakurugenzi.
Waziri huyo pia ameutaka mgodi huo kulipa madeni wanayodaiwa na watumishi zaidi ya Sh 284 milioni, kulipa tozo zote za Serikali wanazodaiwa pamoja na kulipa madeni ya na wanawaosambazia vifaa ‘Suppliers’.
“Hata nikiwafungulia Rais atanishangaa hawa waliiba dhahabu tumewaambia warudishe wameleta utapeli kuleta dhahabu feki, hawa wanadaiwa mamilioni hawajalipa niwafungulie vipi wana madeni na Serikali na suppliers hawajawalipa halafu mnaniambia niwafungulie acha waendelee na ujanja ujanja wao sitawafungulia hadi wakidhi vigezo,”amesema.
Biteko amedai wakurugenzi wa kampuni hiyo wanaishi maisha ya ujanja ujanja na kumtumia mtu anayetumia jina la Rais vibaya kwa kutembea ofisi mbalimbali kuchafua jina la wizara yake na kusema atasimamia sheria na kamwe hatarubuniwa na fedha kufanya jambo kinyume cha utaratibu.