Waziri Lugola Ampa Mwezi Mmoja Kamishna Jenerali Wa Uhamiaji Kuwasaka Madalali Wa Wahamiaji Haramu Nchini Na Nje Ya Nchi


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amempa mwezi mmoja Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI), awasake popote walipo madalali wa wahamiaji haramu waweze kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Lugola alisema lengo la agizo hilo ni kuvunja mtandao mkubwa wa wahamiaji haramu nchini ambao kila mara wanakamatwa lakini bado wahamiaji hao haramu wanazidi kuongezeka.

Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Nchi tatu za Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya na Ethiopia uliofanyika katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, leo, ambao ulikuwa unalenga kuweka mikakati ya kupambana na tatizo la wahamiaji haramu ndani ya nchi hizo, Lugola alisema tatizo hilo ni kubwa Tanzania, Afrika na dunia hivyo lazima wahakikishe wanaliondoa.

Lugola alisema chanzo kikubwa cha tatizo hilo ni kutokana na uwepo wa madalali wa wahamiaji haramu ambao wanafanikisha wahamiaji hao wanasafirishwa kwa wingi katika nchi hizo wakiwahifadhi na kuwasaidia kwenda maeneo ambayo wamepanga kusafiri.

“Mkutano huu ni mkubwa ambapo umeshirikisha nchi tatu ambapo mawaziri wake tupo nao, mkutano huu ni wa juu, ulitanguliwa na mkutano wa wataalamu ambao ulifanyika kwa siku mbili na walifanikiwa kutuletea mapendekezo yao,” alisema Lugola.

Alisema baadhi ya mapendezo ya wataalam hao, ni pamoja na kupambana na biashara hiyo ya wahamiaji haramu, kuona umuhimu wa wahamiaji haramu kutopelekwa mahakanani na kuwafunga magerezani.

“Idadi kubwa ya wahamiaji haramu hapa nchini ni Waethiopia, hivyo wataalam wa mkutano huu walipendekeza kuwepo na mawazo mbadala ambapo wahamiaji hao haramu wanapokamatwa nchini ndani ya siku chache tunawarudisha walipotoka, ambapo Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Wahamiaji (IOM) watasaidia kuwasafirisha katika nchi wanazotoka,” alisema Lugola.

Alisema tatizo la kuwasaka madalali hao si kwa Tanzania tu bali ni kwa nchi zote tatu ambazo watawasaka madalali hao kwa nguvu zote mpaka wahakikishe tatizo hilo limemalizika au kupungua kwa kiasi kikubwa.

“Kuwasaka hawa madalali, sio tu kwa nchi zetu hizi tatu, bali tutawasaka kwa kasi zote mpaka Afrika Kusini, lengo letu kuu ni kuvunja mtandao huu, na kutokana na hilo naomba kuwaonya baadhi ya Watanzania ambao wanawapokea wahamiaji haramu, kuwapa chakula, kuwaficha na kuwahifadhi katika jengo lolote, wenye tabia hiyo nao tutawakamata” alisema Lugola.

Lugola pia alisema licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa za utendaji kazi kutokana na kuwa na ukosefu wa vifaa, aliwapongeza maafisa uhamiaji katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuendelea kufanya kazi nzuri, lakini aliwataka waongeze kasi ya kulinda mipaka usiku na mchana kwa kuwakamata wahamiaji haramu mpaka mtandao huo umalizike.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad