Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuona namna bora ya kuwawisha mitaala ya Chuo hicho ili kifikie viwango vya Elimu ya Juu.
Majaliwa ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo amesema mpaka sasa Chuo hicho kimekidhi viwango vya kuwa na hadhi ya Chuo Kikuu na kwamba elimu inayotolewa katika chuo hicho ndio inasisitizwa nchini.
Aidha Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa kujenga misingi ya Amani, umoja na kuleta maendeleo ya jamii nchini kwa vitendo na kuwataka watanzania kuzingatia maadili, uzalendo na utaifa katika uwajibikaji wa kila siku, kuungana kwa pamoja bila kujali itikadi za kisiasa au kabila katika kulinda na kudumisha tunu hizo.
“Nimpongeze Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi anazochukua ili kuhakikisha anairejesha nchi yetu kwenye misingi yake ya awali ambayo ni kuwa na viongozi waadilifu, wazalendo na wenye kulinda Amani na kudumisha umoja katika jamii, watanzania wote tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi na kuzilinda kwa nguvu zote,” alisema Mhe. Majaliwa.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema ni vizuri kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa ni mtu ambaye amelipigania Taifa na kuliletea ukombozi na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufuata nyayo za Baba wa Taifa.
Waziri Ndalichako ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa wanafunzi katika kongamano hilo kwa kuwa linawapa fursa ya kupata uelewa mpana wa zaidi ya kile wanachofundishwa shuleni, na kwamba taifa linawategema kuwa chachu ya mabadiliko katika nchi.
Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa limechagizwa na mada isemayo Mchango wa Mwalimu Nyerere katika kujenga Amani, umoja na Kuleta Maendeleo ya Jamii nchini.
Waziri Mkuu aeleza umuhimu wa kuwa na Mitaala inayokwenda na mabadiliko
0
April 12, 2019
Tags