Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiwezi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kama ambavyo imependekezwa na baadhi ya Wabunge.
Waziri Mkuu ametoa kauli Bungeni jijini Dodoma kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020 wakati akijibu hoja iliyotolewa kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usisimamiwe na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na badala yake usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Waziri Mkuu amesema serikali inawashukuru Wabunge kwa imani kubwa walioionesha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni huru, juu ya utekelezaji wa majukumu yake, na kuona umuhimu wa kuiongezea jukumu la kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini tume haitosimamia uchaguzi huo.
“Hivyo, jukumu la kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa si miongoni mwa majukumu ya Tume kwa mujibu wa Katiba,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.