Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa agizo kwa maofisa wanyamapori, wanapokamata mifugo itakayokutwa hifadhini, wahakikishe pia wanawakamata wachungaji wa mifugo hiyo.
Amesema hatua hiyo itabadili mfumo wa sasa, ambapo mifugo mingi inayokutwa hifadhini, imekuwa ikikiaatwa bila wachungaji wakidaiwa wamekimbia.
Hatua hiyo inakuja kufuatia tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya maofisa wanyamapori kuwa baada ya kukamata mifugo hiyo ikiwa hifadhini, huwaruhusu wachungaji wakatafute pesa za kuwahonga ili waiachie.
Pale wanaposhindwa kupata pesa walizokubaliana, hushindwa kuirudia mifugo yao kwa hofu ya kukamatwa.
“Wekeni kambi hapo hapo mahali mtakapoikuta mifugo hadi pale mmiliki wa mifugo au mchungaji atakapojisalimisha awe amejificha na kama amepanda juu ya mti mfuateni, ninyi ni askari tuliowaamini,” amesisitiza Kanyasu.
Alitoa agizo hilo wakati alipokuwa akizungumza na mameneja na watumishi wa mapori ya akiba ya Mkungunero na Swagaswaga katika ziara ya kikazi wilayani Kondoa mkoani Dodoma, ambapo alisema shutuma hizo za rushwa zitaisha tu pale watakapokamata mifugo na wachungaji wake.
Alisema hadi hivi sasa kuna mifugo zaidi ya 200 katika Pori la Akiba la Mkungunero pekee, ambayo imekamatwa na haijulikani kuwa ni mali ya nani.
“Jambo la kujiuliza ni mifugo hiyo ilikuwa ikijichunga yenyewe?” alisema.
Alisema “Sitaki kusikia kuanzia sasa eti mmeikamata mifugo bila mchungaji au mmiliki, hakikisheni mnapiga kambi hapo hata ikiwa wiki mbili hadi pale mmiliki atakapojitokeza ili mkamate yeye pamoja na mifugo yake.
“Serikali imewagharamia kuwapa mafunzo ya kijeshi ya namna ya kupambana na wahalifu halafu unaniambia kuwa wachungaji wa mifugo hiyo mara baada ya kuwaona hukimbia kwa kupanda juu ya miti, kwanini na wewe usipande huko huko?” amehoji.