Waziri wa ulinzi aliyeapishwa kuwa rais wa mpito Sudan Ahmed Awadh Auf, amejiuzulu wadhifa huo, sababu zaelezwa
0
April 13, 2019
Waziri wa ulinzi aliyeapishwa Alhamisi kuwa rais wa baraza la mpito la kijeshi Ahmed Awadh Auf amejiuzulu wadhifa huo jana(12.04.2019) na nafasi yake kuchukuliwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan Abdulrahman.
Sudan Vizepräsident Awad Ibn Auf (picture-alliance/Xinhua/M. Khidir)
Kwa mujibu wa dw Swahili. Awadh Auf ametangaza hatua hiyo siku moja baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais al-Bashir na yeye kushika hatamu.
Kwenye hotuba yake ya kujiuzulu, iliyorushwa kwenye televisheni Awadh Auf alisema anaachia wadhifa huo kwa maslahi ya taifa na kwa kuwa taifa hilo lina watu wazuri na jeshi la kuaminika. Amesema ana imani kwamba makundi hayo mawili yatafanya kazi pamoja. Auf ambaye anakabiliwa na vikwazo kutokana na ushiriki wake kwenye mauaji hayo alikuwa akikabiliwa na shinikizo la kimataifa akitakiwa kuanzisha serikali ya mpito ya kiraia.
Mapema jana, jeshi liliwahakikishia raia kwamba halina mpango wa kuongoza kwa muda mrefu. Baraza hilo pia lilisema utawala wa kijeshi wa miaka miwili ya mpito unaweza kubadilishwa na kuahidi kwamba linaweza kuvunjwa muda mfupi ujao iwapo kutafikiwa suluhu la mzozo wa kisiasa unaolikabilia taifa hilo.
Demonstration Sudan Karthoum (Reuters)
Raia walikusanyika tena Ijumaa kushinikiza serikali ya kiraia
Raia walionekana kufurahishwa na hatua hiyo ya ghafla ingawa mapema jana jeshi liliwahakikishia kwamba halina nia ya kutawala moja kwa moja. Awadh Auf alikula kiapo cha kuongoza baraza hilo la mpito usiku wa Alhamisi muda mfupi tu baada ya rais al- Bashir kupinduliwa na kukamatwa.
Kuondolewa kwa Bashir kulifuatia miezi kadhaa ya maandamano yaliyokuwa yakiipinga serikali, lakini hata hivyo waandamanaji walisema hawakufurahishwa kuona nafasi yake inachukuliwa na waziri wa ulinzi ambaye ni sehemu ya serikali yake iliyodumu kwa muda mrefu.
Kundi linaloratibu maandamano hayo limesema kupitia ukurasa wa Facebook kwamba kujiuzulu kwa Auf ni ushindi kwa matakwa ya raia. Aidha limeijibu hatua hiyo kwa kuapa kwamba waandamanaji wataendelea kusalia mitaani hadi kutakapopatikana serikali ya kiraia.
Mapema jana Ijumaa, baraza la Usalama la Umoja wa mataifa lilifanya mkutano wa ndani, kufuatia ombi la Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Ubelgiji na Poland. Balozi wa Ujerumani kwenye Umoja wa Mataifa Christoph Hausgen aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo kwamba kunatakiwa kuwepo na mchakato wa kisiasa ulio wa haki na jumuishi.
Aidha ametaka al-Bashir kwenda mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC akisema mataifa yanawajibika kumkabidhi The Hague. Baraza hilo litakutana tena Jumatatu kujadiliana kuhusu hali itakavyokuwa nchini humo.
By Ally Juma.
Tags