Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto imesikitishwa na vitendo vya baadhi ya wanawake wanaoendelea kutelekeza watoto.
Akiwa Mkoani Njombe katika Hospital ya rufaa Kibena Mkoani humo Waziri wa Wizara hiyo Ummy Mwalimu ameonyesha kutopendezewa na tabia hiyo baada ya kukutana na kichanga mwenye afya na siha njema anayeendelea kulelewa hospitalini hapo baada ya kuokotwa siku chache zilizopita pembezoni mwa barabara kata ya Mji Mwema Mjini Njombe.
"Jamani inasikitisha sana sisi binaadam kutupa watoto wazuri kama hawa,halafu mtoto ni mzuri anafuraha jamani hii sio tabia Njema kabisa," alisema Ummy.
Kwa upande wake katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula ametoa wito kwa akina mama kuwapenda na kuwalinda watoto wao, aidha ili kuonyesha namna anavyojali na kuwapenda watoto ameahidi kumchukua kumlea na kumtunza mtoto huyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy alipofika katika wodi ya wazazi amewapongeza wakina mama walioweza kujifungua salama huku akisisitiza kuendelea kupokea mafunzo ikiwemo uzazi wa mpango.
Wizara ya Afya Yalia na Kina Mama Wanaotupa Watoto Wachanga
0
April 09, 2019
Tags