MTWARA, Tanzania - Young Africans imeshindwa kutamba mbele ya Nangwanda Sijaona mjini Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kubanwa mbavu kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1.
Yanga waliokuwa wenyeji walianza kufungwa bao la kwanza kupitia mnamo dakika ya 19 kwa Vitalis Mayanga aliyemzidi ujanja beki Kelvin Yondani kisha kumpiga chenga kipa Klaus Kindoki na kupasia mpira nyavuni.
Ilichukua dakika moja pekee kwa bao hilo na katika dakika ya 20 Yanga walipata penati baada ya mshambuliaji wake, Heritier Makambo kuangushwa kunako eneo la hatari na mchezaji wa Ndanda.
Penati hiyo ilishindwa kuzama nyavuni baada ya mpigaji, Mrundi, Amis Tambwe, kupiga mpira ulioenda nje ya lango la Ndanda na kumsaidia kipa wake Said Nduda ambaye alikuwa ameelekea upande tofauti.
Mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika, Ndanda walikuwa kifua mbele kwa bao hilo moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Yanga wakijaribu kufanya jitihada za kutafuta bao la kusawazisha ambazo zilizaa matunda mnamo dakika ya 61 kwa Papy Tshishimbi kuisawazishia kwa njia ya kichwa nkupitia mpira wa krosi uliopigwa kushoto mwa uwanja.
Bao la Tshishimbi lilidumu mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika kwenye Uwanja huo, matokeo yakiwa ni 1-1.
Katika kipute hicho, Kocha Mwinyi Zahera aliwafanyia mabadiliko baadhi ya wachezaji wake kipindi cha pili kwa kumtoa Tambwe na kumuingiza Deus Kaseke, pia Jaffary Kibaya na kumuingiza Rafae Daudi.
Msimamo wa ligi hivi sasa unaonesha kuwa Yanga bado ipo kileleni ikiwa na alama 68 baada ya kuongeza moja leo huku Ndanda wakifikisha alama 37 kwenye nafasi ya 15.