Askari mmoja wa jeshi la Magereza, aliyetambulika kwa jina la Kibemba Warioba (27) mwenye namba B.9205 WDR amekamatwa na jeshi la polisi mkoa wa Mwanza kwa kosa la kuanzisha SACCO’s yenye jina la Info Tell CCM na kuwatapeli wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, leo Mei 26, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jumanne Murilo amesema askari huyo alikamatwa jana Mei 25, 2019 baada ya kupokea taarifa kwa wanachama wa CCM kwamba kuna saccos ya info Tell CCM inayotoa gawio kwa wanachama wa chama hicho.
“Askari huyo alikuwa anafanya kazi katika gereza la Biharamulo mkoani Kagera, kabila lake ni mzanaki, mpaka sasa tunavyozungumza na nyinyi tayari tumewasiliana na viongozi wa jeshi la magereza na amesimamishwa kazi ili kuendelea na uchunguzi na kumfikisha mahakamani.. Shughuli hii si kwamba alikuwa anaifanya yeye mwenyewe bali na watu wengine na baadhi yao tumewakamata ambao wamewatapeli wanachama wa CCM wakiwaeleza kuwa watapata gawio zuri na maisha yao yatakuwa mazuri na bora.” amesema Kamanda Murilo na kukazia kuhusu kukamatwa kwake.
“Mtumishi huyu ameichafua sura ya jeshi la magereza, serikali na jina la chama cha CCM, hatuwezi kuvumilia watu wa aina hii kuendelelea kufanya uhalifu na utepeli, tutawashughulikia na kama kuna watu wenye nia ya kujihusisha na shughuli isiyo halali ni vema wakaiacha,”amesema Kamanda Murilo.
Kwa upande mwingine, Kamanda Murilo amesema baada ya taarifa hiyo kupokelewa, askari wa Mwanza walishirikiana na askari wa Mkoa wa Kagera walimfuatilia askari huyo na kufanikiwa kumkamata akiwa na laini za simu 5 zikiwa zimesajiliwa kwa majina tofauti.
Ameeleza kuwa, baada ya uchunguzi dhidi ya askari huyo wa magereza alikiri ndiye mhusika na tayari amewatapeli wanachama wa CCM kwa kujitambulisha kwa vyeo mbalimbali vilivyopo ndani ya CCM.
Askari Magereza awatapeli wanachama wa CCM kupitia SACCO’s
0
May 27, 2019
Tags