Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe amehoji juu ya kutoonekana kwa mwanamke anayedaiwa kufanya tendo la ndoa na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajima na kusema suala hilo lilikuwa na nia ovu.
Askofu Kakobe ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akizungumza kwenye ibada maalum iliyoandaliwa na Askofu Gwajima ambayo ililenga kuelezea kiundani zaidi kuhusiana kusambaa kwa video ya ngono inayomdhania kumuhusisha mtu anayefanana na Mchungaji huyo.
"Mshtaki wa Josephat Gwajima yuko wapi, ndiyo sasa hivi polisi wanahangaika kumtafuta amejificha mafichoni, sasa wewe una hoja ya kweli unajificha nini?, unachojificha ni nini wakati hii tuhuma umeihakikisha na unataka Gwajima ashughulikiwe, Yesu anauliza mshtaki wako Gwajima yuko wapi? mbaya zaidi nilivyoambiwa kwenye video hata sura ya mwanamke aliyetembea na Gwajima haonekani, sura yake imefichwa." amesema Kakobe.
"Kuna mwongozo ambao biblia unatutaka kuufuata yupo mchungaji mmoja ambaye tuhuma nyingi zilinifikia, kama Askofu Mkuu wakasema huyu anafanya uzinzi sana lakini kukawa hakuna ushahidi wanaoweza kuthibitisha, bila shaka nikawaambia mashtaka juu ya mzee hayawezi kukubalika nikawaambia watengeneze mtego, ili wamnase vizuri." ameongeza Kakobe.
"Walifanikiwa wakampata vizuri wakapiga picha nzuri za video na mnato, wakeleza mwanzo mpaka mwisho kiasi kwamba yule ambaye alishtakiwa alishindwa kujitetea na hapo ndipo tulipochukua hatua na yule tukamtenga kanisani, na kanisa langu wanajua hatuna mchezo katika hili". ameongeza Kakobe.
Mapema wiki iliyopita kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, kulisambaa kipande cha video ambacho kilidaiwa kumuonesha Mchungaji Gwajima akifanya tendo la ndoa na mwanamke lakini Askofu Gwajima mwenyewe alikanusha taarifa hiyo na kueleza kuwa imelenga kumchafua kwa kuwa uchaguzi umekaribia.