Askofu Nkwande Akemea Uchawi, Ushoga Na Utoaji Mimba.....Asema Ni Ushamba Wa Elimu, Ni Uuaji, Ni Dhambi

ASKOFU MKUU wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhasahamu Renatus Nkwande anasikitika kila anaposikia watu wanaongelea mambo ya uchawi na kusema kwamba huo ni usahamba wa elimu.

“Mtu akivimba tumbo unasema amelogwa na tena unamtaja na fulani ndiye mchawi. Huo ni ushamba wa elimu na tena huko ni kukosa imani na kushindwa kumuamini Mwenyezi Mungu,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Mei 12, 2019) wakati akitoa shukrani kwenye ibada ya kumsimika kuwa Askofu Mkuu wa jimbo hilo iliyofanyika kwenye viwanja wa Kawekamo jijini Mwanza.

“Watu wetu wana hofu mbalimbali ambazo zimewakamata tangu utoto wao. Tuwasaidie waumini hawa ili wamwamini Mungu kwamba anaokoa na anaweza kuwaponya madhila waliyonayo. Tuwasaidie watu wetu wajikomboe kielimu, wajiendeleze kwenye masomo ya fizikia, kemia na kadhalika,” amesema.

Amesema anashangaa tabia ya Waafrika ya kupenda kuiga mambo ya ajabu kwa vile tu yameletwa na wazungu. “Sisi Waafrika ni watu wa ajabu tunaiga vitu visivyo na msingi. Wameleta ushoga, tunaiga! Wameleta utoaji mimba, tunaiga. Leo hii kuna taasisi zinasambaza hata vifaa vya kutolea mimba, nasi tumekaa tunaangalia tu.”

“Wazee wetu walipoona wamechoka ukoloni, walipigana ili kupata uhuru. Leo na sisi tupiganie uhuru kwa kukataa masuala ya ushoga na utoaji mimba. Huo ni uuaji, hiyo ni dhambi. Miongoni mwetu leo wapatikane watu wa kusimamia hayo ili ukoloni huu usiendelee kutawala akili za watu wetu,” amesema.

Amewaomba Watanzania wamuombe Mungu awabariki, alibariki Taifa la Tanzania ili yanayofanyika yawasaidie kwenda mbinguni.

Pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo na hatimaye kuwatoa kwenye umaskini. “Tunaamini yote anayofanya ni kwa manufaa ya Watanzania wote,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Magufuli na mamia ya waumini na viongozi waliohudhuria ibada hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema anatambua kuwa kuwaongoza watu kiroho na kimwili ni jambo lenye uzito mkubwa. Na kwamba uteuzi wake unadhihirisha kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kumtumikia Bwana.

“Sisi viongozi na waumini kwa kutambua kazi nzuri uliyoifanya hadi kufikia kupata wadhifa huo tuna imani utaweza. Nakuomba upokee mzigo huo kwa matumaini na bila kusita kwani waumini wa kanisa hili wako pamoja nawe na viongozi wenzako wote tunategemea watatoa ushirikiano kwako. Tunachosema ni kwamba, jipe moyo kwa kuzingatia yaliyoandikwa katika Wafilipi 4:13 kwamba “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. Jitwishe mzigo huo kwa imani na utaubeba bila kuchoka, sisi sote tuko pamoja nawe,” amesema.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kusisitiza suala la kutunza amani ya nchi na akawaataka viongozi wa dini na waumini kote nchini kuendeleza upendom hurma na kuwa na roho ya msamaha. “Tuhurumiane sasabu sisi si wakamilifu, kwa hiyo tuongeze msamaha miongoni mwetu,” amesisitiza.

“Nawaombeni wote, tuendelee kutumia nyumba zetu za ibada kuliombea Taifa hili ili tuendelee kuishi kwa amani, upendo na mshikamano. Tuepuke migogoro ya mara kwa mara katika nyumba zetu za ibada. Tuendelee kujenga waumini wetu wakue kiroho na kujenga dhana ya umoja na upendo katika Taifa letu. Watu wa Mungu ni watu wa upendo, watu wa Mungu ni watu wa amani, watu wa Mungu ni watu wa kiroho.”

Mapema, akitoa salamu za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Rais wa TEC, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga aliwataka waumini wa kanda ya ziwa wawe na mshikamano na wampe ushirikiano Askofu Mkuu Nkwande.

“Kuweni na upendo kama Bwana Yesu alivyofundisha na pia ombeeni utumishi mwema kwa viongozi wote wa Serikali na watumishi wote wenye jukumu la kuongoza watu.”

Askofu Nyaisonga aliishukuru Serikali kwa kulipa nafasi Kanisa Katoliki ya kushirikiana na Serikali kutoa huduma za jamii kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini hususani katika sekta ya elimu na afya.

“TEC inapenda kuhimiza mshikamano baina ya Serikali na kanisa ili kuwe na ufanisi wa huduma tunazotoa za kumlinda mama na mtoto na kijana. Ufanisi huu utapatikana kwa kuimarisha miundombinu hasa katika ngazi za chini,” alisema.

Waziri Mkuu ameondoka jijini Mwanza mchana huu kuelekea Arusha kupokea kundi la watalii zaidi ya 200 kutoka China ambao wanatarajiwa kuwasili leo jioni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad