Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imepokea jumla ya Sh19 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia za maeneo yaliyotwaliwa na jeshi.
Hata hivyo, ni Sh3 bilioni ndizo zilizolipwa hadi sasa huku Sh16 bilioni zikisubiri uhakiki ili kukamilisha malipo hayo kwa ardhi ya wananchi.
Akijibu swali bungeni leo Jumatano Mei 15, 2019, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussen Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuwalipa wananchi fidia katika maeneo ambayo yalichukukiwa kwa shughuli za Jeshi.
Kauli ya Dk Mwinyi imekuja ikiwa ni siku chache tangu msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alipotangaza wananchi wote wanaoishi katika maeneo ya Jeshi kuhama haraka vinginevyo wataondolewa kwa nguvu.
Mbunge wa Mtambile (CUF) Masoud AbdallaH Salim amehoji Serikali ina mpango gani wa haraka wa kulipa fidia kwa wananchi waliochukuliwa maeneo yao na Jeshi.
"Ni kweli yapo maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya ulinzi wa mipaka lakini baadhi ya maeneo yamelipwa fidia na mengine bado mchakato unaendelea," amesema Mwinyi.
Waziri Mwinyi amesema mpango wa Serikali ni kuendelea kulipa fidia kwa maeneo husika na mwaka 2018/19 wizara ilitenga Sh20.9 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia hiyo lakini zilizotolewa ni Sh19 bilioni.
Bilioni 19 Zatengwa kwa ajili ya kulipa fidia za maeneo yaliyotwaliwa na jeshi.
0
May 16, 2019
Tags