Dk. Shein atoa neno kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein amewanasihi wafanyabiashara kuwa waadilifu katika kuwafanyia wanunuzi tahafifu za bei za bidhaa na huduma nyenginezo hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo katika risala maalum aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari katika kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu wa 1440 Hijria sawa na mwaka 2019 Miladia.

Katika risala yake hiyo, Alhaj Dk. Shein aliwataka wafanyabiashara kukumbuka kwamba kwa kufanya hivyo hawatokula hasara bali watazidi kupata fadhila mbali mbali za Mola wao Mlezi zinazoambatana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Aidha, aliwataka wakulima waendelee na ustaarabu pamoja na utamaduni wao ule ule wa ustahamilivu na uadilifu kwa kujiepusha na tabia ya uvunaji na uuzaji wa mazao machanga.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar si kumkomoa mtu kwa sababu Serikali huwa haiwakomoi wananchi wake bali dhamira yake ni kuwalinda na kuona kwamba hawafikwi na matatizo ambayo yanaweza kuepukika na kujikinga nayo.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa nasaha zake kwa wale ambao si Waislamu na wale ambao watakuwa na dharura zinazowazuwia wasifunge kuwa wasifanye vitendo vitakavyoathiri wanaofunga.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad