Hivi Ndivyo Ukahaba Unavyofanyika Kupitia Simu na Mitandao ya Kijamii Hapa Tanzania
0
May 10, 2019
Wakati polisi wakikimbizana na makahaba wanaojiuza katika maeneo mbalimbali maarufu na klabu za usiku, biashara hii sasa imehamia katika mitandao ya kijamii.
Biashara hiyo ambayo awali ilikuwa ikifanyika katika viambaza vyenye mwanga hafifu katika maeneo maarufu, sasa inafanyika kwa uwazi katika mitandao.
Gloria, mmoja wa wanawake ambao kwa zaidi ya miaka 20 amefanya biashara hiyo anasema: “Biashara imebadilika sana, huhitaji kutumia nguvu nyingi au kutangatanga kupata mteja... unaingia tu mtandaoni wamejaa tele.” Mwanamke huyu anasifu ukuaji wa teknolojia akisema umeisaidia biashara hiyo kwani pamoja na kuirahisisha, pia umeipa thamani kwa kuwa bei ya mtaani na mtandaoni ni tofauti kabisa.
Jinsi inavyofanyika
Kwa mujibu wa Annie Jameson (siyo jina lake halisi) biashara hii hufanyika kupitia tovuti mbalimbali (dating sites), mitandao ya kijamii kama badoo, facebook, wechat na ile ya simu za mkononi BBM, WhatsApp na telegram.
Anasema watumiaji hutofautiana kutokana maeneo walipo, akitolea mfano hapa nchini alisema: “Bado wanunuzi na wauzaji hawatumii dating sites kwa sababu utaingia kwenye matatizo na Serikali. Wenzetu wamefikia hatua hiyo lakini hapa mitandao tunayotumia ni ile inayopunguza wigo wa taarifa kusambaa kwa uwazi,” anasema.
Alisema ingawa biashara hiyo imeshamiri nchini lakini inafanyika kwa ustadi ili wasiharibu soko hasa kwa wanaume ambao ndiyo wateja wao.
“Unajua wanaume wanapenda sana hivi vitu lakini wanataka kulinda heshima zao, kwa hiyo ukijiweka kwenye dating sites inakuwa ngumu kidogo kukufuata, lakini kwenye WhatsApp au BBM ‘fastaa’ wanakuja,” alisema. Biashara hiyo kupitia WhatsApp imechukua kasi zaidi kutokana na kuwapo kwa mtu wa kati (supplier) ambaye anakuwa na wasichana zaidi ya 20 ambao anakuwa na picha zao kwa ajili ya wateja wanaowahitaji.
Kwa kutumia mtandao huo, mteja anapotaka msichana huomba kwa ‘supplier’ atumiwe picha ili achague anayemtaka.
“Ni rahisi siku hizi wala huhangaiki kama una hela unapata picha unachagua halafu unaeleza ulipo anakuja kwa gharama ya kuanzia Sh20,000 mpaka Sh100, 000 inategemea tu kiwango cha msichana mwenyewe na nguvu yako katika kuomba punguzo,” alisema mmoja wa wateja na kuongeza:
“Masupplier wapo kibao siku hizi hata ukiwa mkoani unaweza kuwasiliana na ambaye unamjua Dar es Salaam unashushiwa tu kazi.”
Mteja mmoja ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema alikuwa hajui anawezaje akapata wanawake wanaojiuza kwa njia hiyo hadi alipoelezwa na marafiki zake mtaani.
“Palepale akanionyesha na kuniunganisha na mwenye mademu kisha nikamrushia supplier Sh10,000 halafu nikaletewa picha zaidi ya 10 nikachagua na kuelekeza nilipo, demu akaja na pikipiki hadi pale tulipokuwa kazi ikawa imeisha.”
Alisema gharama ya huyo msichana mwenyewe ilikuwa ni Sh100,000 lakini akitaka apate kinywaji au chochote gharama zitakuwa juu ya mteja.
“Gharama nyingine ni zako mwenyewe anakuja kwa shughuli moja tu,” alisema.
Kinachoendelea mitandao mingine
“Naitwa Baker, nahitaji jimama kama wewe wa kunilea mimi nitakupa mapenzi hadi uchoke, namba zangu hizo 071......(anaziandika). Hivyo ndiyo ulivyoanza ujumbe katika mtandao wa marafiki wa Badoo. Mbali ya mtandao huo, mabinti wengi, hasa wa vyuo wameanzisha akaunti katika mitandao mbalimbali ikiwamo Facebook, Twitter, Instagram, Imo na mingine mingi kwa ajili ya kunadi biashara ya ngono.
Mitandao mingine inayotumika katika biashara hiyo ni Tinder, Lovoo, SpeedDate, BeNaughty, Are You Interested na SayHi. Mitandao hii si tu huwakutanisha wanawake hao na wanaume wa ndani, bali hata wa nje ya nchi hasa kwa wale wanaotafuta Wazungu.
Msichana mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema amesafiri kwenda nchi mbalimbali zikiwamo Kenya, Ghana na Marekani kwa shughuli za ngono baada ya kukutana na wanaume kwenye mitandao hiyo na kukubaliana.
Alisema amewahi kuwakutanisha rafiki zake zaidi ya 10 katika mitandao na kuangalia umbali wa wanaume wanaozungumza nao na kuoanisha na maelezo.
“Kuna mitandao, ukiwamo SayHi!, inakupa hadi ramani huyo mtu alipo. Hii inakusaidia kujua taarifa za mteja unayechati naye kwa kuwa wengine huwa waongo,” alisema.
Msichana huyo alisema mbali na kwenda nchi za nje, hapa Tanzania amekwenda katika mikoa mingi kufuata wateja wa ngono, Zanzibar ikiongoza.
Mmoja wa wanaume wanaotumia mitandao kusaka ngono, alisema: “Nilikutana binti mtandaoni, nikamfuatilia, tukakutana naye maeneo ya Duce (Chang’ombe, Dar es Salaam), tukaenda Keko, nimekuwa naye hadi asubuhi hii, nimempa Sh50,000 kama tulivyokubaliana.
“Alitaka 150,000 na alivyovaa, ningekuwa nayo ningetoa nilivyomwambia sina tupange siku nyingine akaniuliza nina ngapi nilipomwambia nina Sh50,000 tu aliniambia lete hiyohiyo kwa leo,” alisema kijana huyo.
Kijana mwingine, Abdulrazaq Ibrahimu amewahi kukutana na wasichana wengi mtandaoni lakini tofauti na wengine, alikuwa akifanya utafiti akitaka kufahamu jinsi biashara ya ngono inavyohusisha watu wa hadhi, vyeo, umri na madaraja tofauti.
Alisema kati ya wasichana wasiopungua 25 aliokutana nao mtandaoni, hakuna aliyemkawiza eneo la miadi kwa muda mrefu. Wapo aliowakuta wamefika na wengine wakifika baada tu ya kuwaambia amefika eneo husika.
Tags