Jeshi la Israel linasema limemuuwa kamanda wa ngazi za juu wa kundi la Hamas kwenye mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza, huku pande zote mbili zikiapa kuendelea na mapigano.
Taarifa ya pamoja kati ya jeshi na shirika la ujasusi la Israel, Shin Bet, inasema kamanda huyo, Hammed Al-Ghudari, alikuwa anahusika na kusafirisha fedha kutoka Iran kuyapelekea makundi ya wanamgambo kwenye Ukanda wa Gaza. Mashahidi wanasema aliuawa kwa shambulio la anga akiwa kwenye gari yake siku ya Jumapili (Mei 5). Wizara ya Afya ya Palestina ilithibitisha kifo hicho.
Hayo yanajiri huku idadi ya raia wa Israel waliouawa na maroketi yaliyorushwa kutoka Gaza ikifikia wawili na mwengine wa tatu akiripotiwa kuwa hali mbaya.
Maroketi yalikishambulia kiwanda kimoja kwenye mji wa Ashkelon na gari moja katika kijiji cha Kibbutz Yad Mordechai, huku kipande cha roketi jengine kikitua na kuharibu hospitali moja mjini Ashkelon, ingawa hakuna majeruhi walioripotiwa.
Kwa upande wa Wapalestina, mbali na Ghudari, wapiganaji wengine wawili waliuawa kwa mashambulizi ya anga ya Israel mashariki mwa Gaza, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema kwamba ameliagiza jeshi kuongeza mashambulizi yake kuelekea Ukanda wa Gaza.
Netanyahu aliamuru kutumwa kwa magari zaidi ya kijeshi, mizinga na kikosi cha wanajeshi wa ardhini na alitoa wito wa mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya kile alichokiita makundi ya kigaidi, kwa mujibu wa taarifa ya ofisi yake.
Mahmoud al-Zahar, kiongozi wa ngazi za juu wa Hamas, aliwaambia waandishi wa habari kwamba wasingealiacha kushambulia na kwamba walikuwa wanafuta makubaliano ya kusitisha mapigano baina yao na Israel.
Jeshi la Israel lilisema kwamba kufikia Jumapili mchana lilishalenga shabaha 260 dhidi ya makundi ya wanamgambo mjini Gaza, huku wanamgambo hao wakirusha makombora na maroketi 450 ndani ya Israel tangu siku ya Jumamosi.
Usiku wa Jumamosi, raia mmoja wa Israel aliuawa, huku raia watatu wa Kipalestina, akiwemo mwanamke mja mzito na mtoto wake, waliuawa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina. Wapiganaji wengine wanne wa Kipalestina waliuawa siku ya Jumamosi.
Hata hivyo, jeshi la Israel limekanusha kuhusika na kifo cha mwanamke huyo mjamzito na mtoto wake mwenye umri wa miezi 14, likisema wahanga hao waliuawa kwa roketi lililopotea njia kutoka upande wa Hamas.
Shirika la uokozi la Israel, Magen David Adom, lilisema kuwa liliwatibu zaidi ya watu 80, wengine wakiwa na majeraha kutokana na vipande vya maroketi, huku wengine wakiwa na majeraha yaliyotokana na kukimbilia maeneo salama. Wengi zaidi ni wale waliopata mshituko.
Makabiliano haya ya sasa yanakuja baada ya Wapalestina wanne kuuawa na wengine 51 kujeruhiwa na jeshi la Israel mpakani mwa pande hizo mbili siku ya Ijumaa. Wawili kati ya hao, walikuwa wanamgambo wa Hamas, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina.
Israel, Hamas Waendelea Kudundana Kwa Makombora na Ndege za Kivita
0
May 06, 2019
Tags