Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kupewa vifaa na zana bora za kisasa.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussen Mwinyi, amesema katika mwaka ujao wa fedha 2019/20, watalipa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vifaa na zana bora za kisasa.

Alisema sambamba na hilo, watatoa mafunzo kwa wanajeshi ili kuliongezea jeshi hilo uwezo na weledi wa kiutendaji, kiulinzi na kivita.

Akiwasilisha hotuba ya wizara hiyo bungeni jana, Dk. Mwinyi alisema pia wamepanga kuboresha mazingira ya kazi, kuimarisha upatikanaji wa huduma stahiki na mahitaji ya msingi kwa wanajeshi na watumishi wa umma.

Pia, kuwapatia vijana wa Tanzania mafunzo ya ukakamavu, umoja wa kitaifa, uzalendo na stadi za kazi.

Aidha waziri huyo alieleza kuwa wizara itaendeleza tafiti na uhaulishwaji wa teknolojia kwa kuimarisha na kuanzisha viwanda kwa madhumuni ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia.

Pia kuimarisha ushirikiano wa jumuiya za kimataifa, kikanda na nchi moja moja katika nyanja za kijeshi na kiulinzi.

Nyingine ni kufanya upimaji, uthamini na ulipaji fidia ya ardhi katika maeneo yaliyotwaliwa kwa matumizi ya jeshi.

Dk. Mwinyi aliongeza kuwa wataendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura pale inapohitajika.

“Kulipa stahili mbalimbali za maafisa, askari, vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa na watumishi wa umma.

“Kukamilisha sera ya ulinzi wa taifa, mwongozo wa viwanda jeshini na mpango wa maendeleo wa miaka 10, yaani 2018/29-2027/28 wa kuliimarisha Shirika la Nyumbu,” alisema.

Dk. Mwinyi pia alizungumzia hali ya usalama wa mipaka ya Tanzania kuwa ipo shwari licha ya kuwapo tishio kutoka kwenye vikundi vya kigaidi katika baadhi ya nchi jirani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad