Kenya ‘yalamba dili’ kufundisha Kiswahili shule za Afrika Kusini
0
May 20, 2019
Serikali za Kenya na Afrika Kusini zimesaini makubaliano (MoU) ya kufundisha Kiswahili kama somo kwenye mfumo wa elimu wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika.
Kupitia makubaliano hayo, Kenya imepata fursa ya kupeleka wakufunzi wake nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kufundisha lugha hiyo adhimu iliyozaliwa katika Pwani ya Afrika Mashariki.
Katibu wa Elimu wa Baraza la Mawaziri la Kenya, George Magoha alisaini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali ya nchi hiyo na Angelina Matsie Motshekga, Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini alitia saini kwa niaba ya Serikali ya nchi yake.
Makubaliano hayo yanaipa Kenya fursa ya kutumia uwezo wake wa elimu za sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini.
Akizungumza wakati wa makubaliano hayo, Magoha ameeleza kuwa lugha ya Kiswahili itakayoanza kufundishwa kwenye mfumo wa shule za Afrika Kusini itaimarisha ushirikiano kati ya watu wa nchi hizo.
Kwa upande wa Motshekga, alisema kuwa makubaliano hayo ni fursa muhimu kwa Wakenya kwani asilimia 40 ya watu wanaosoma kwenye viwango mbalimbali vya elimu nchini Afrika Kusini wanazungumza Kiswahili.
Makubaliano hayo yatawapa wanafunzi nafasi ya kufanya machaguo ya kusoma Kiswahili kama mbadala wa somo la lugha ya Kifaransa na Kireno.
Kuna watu milioni 5 duniani kote ambao wanazungumza Kiswahili kama lugha yao ya kwanza (lugha ya mama), na watu zaidi ya milioni 135 wanaoizungumza kwa ufasaha kama lugha yao ya pili. Idadi kubwa ya wanaozungumza lugha hiyo kwa ufasaha inatoka nchini Tanzania.
Tanzania, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni nchi ambazo Kiswahili kinatambulika kama lugha ya Taifa.
Tanzania ambao ni kinara wa Kiswahili, tumekwama wapi kuzipata fursa za kusambaza lugha hii? Tunakwama wapi?
Tags