Meya wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema chama hicho kwa sasa kimetoa ruhusa ya kuwapokea baadhi ya waliokuwa wanachama na viongozi wake ambao walikihama chama hicho kuelekea vyama vingine ikiwemo CCM.
Meya Jacob ametoa kauli hiyo alipokuwa akimpokea kada wa Chama Cha Mapinduzi Gonga Kidera, ambaye zamani alishawahi kuwa kiongozi ndani ya CHADEMA, lakini alihamia CCM ili kumuunga mkono Rais Magufuli.
Akizungumza kwenye mkutano huo Meya Jacob amesema kuwa "mwanzoni chama kilikataa lakini sasa hivi kimekubali, ndiyo maana mnamuona Kidera sasa hivi yuko hapa, huyu ni moto ametoka CCM asubuhi na sasa hivi amejiunga na chama chake cha zamani."
"Sio huyu tu yupo jamaa mmoja alishawahi kuwa kiongozi wa chama fulani cha upinzani akahamia CCM, baada ya kuridhishwa na kazi nzuri ya Rais Magufuli, huyu ambaye simtaji lakini ametufuata akituomba ushauri baada ya kuona chama chake cha zamani hakieleweki tukamwambia aje hatuna tatizo naye muda ukifika nitamtaja." ameongeza Meya Jacob.
Mara ya mwisho mwanasiasa maarufu ambaye alifanikiwa kujiunga na chama hicho ni aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu, ambaye alijiunga Novemba 19, 2017, kwa kile alichodai kuwa ni kutokuwepo kwa demokrasia.