Kimenuka..Shamim Mwasha, Mumewe Mbaroni Dar Tuhuma Dawa za Kulevya

Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) imemkamata mfanyabiashara, Abdul Nsebo maarufu Abdukandida na mkewe, Shamim Mwasha kwa tuhuma ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin.

Wanandoa hao wanadaiwa kukutwa na dawa hizo zenye uzito wa zaidi ya gramu 400 nyumbani kwao Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Kamishna wa operesheni wa DCEA, Luteni Kanali Fredrick Milanzi amelieleza Mwananchi kuwa, watuhumiwa hao walikamatwa Mei Mosi mwaka huu.

Amesema kukamatwa kwa Nsebo na mkewe kumekuja baada ya kukamatwa kwa mtandao mkubwa wa dawa hizo hivi karibuni.

Amesema maofisa wa DCEA baada ya kupata taarifa walienda nyumbani kwa watuhumiwa hao na kufanya upekuzi na kubaini mfuko ukiwa na dawa hizo za kulevya na nyingine zilikutwa katika siti ya nyuma ya gari.

"Tulifanya upekuzi kuanzia saa 8:00 usiku hadi saa 1:00 asubuhi na tulizibaini dawa hizo zikiwa zimefichwa na matokeo ya awali kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali yameonyesha ni dawa za kulevya aina ya heroin.”

“Vitu vingine tulivyomkuta navyo ni simu tano, kadi za benki, hati ya kusafiria pamoja na nyaraka mbalimbali ambavyo vyote tumevichukua,” amesema Luteni Kanali Milanzi

Amesema watuhumiwa hao wana mtandao mkubwa wa kimataifa na kwamba wana majina ya watu wanaoshirikiana nao kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Brazil.

Amesema wawili hao bado wanashikiliwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad