WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, ameweka wazi kwamba kabla ya kufanyika uchaguzi wa Klabu ya Yanga jana Jumapili, alishawahi kupigiwa simu na watu wengi ambao wengine walimpa lugha kali zisizoelezeka ikiwa ni baada ya viongozi waliokuwepo madarakani akiwemo mwenyekiti Yusuf Manji, kujizulu.
Mkuchika alikuwa mmoja wa wanachama wa Yanga ambao walijitokeza jana katika uchaguzi mkuu wa Yanga wa kuwachugua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe uliofanyika katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar.
Yanga ilifanya uchaguzi wake ikiwa ni baada ya viongozi wa klabu hiyo wakiongozwa na Manji, makamu mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wa kamati ya utendaji kujiuzulu nafasi zao.
Mkuchika amesema kwamba alikuwa anatolewa lugha hizo kali kupitia njia ya simu wakati ambao klabu hiyo haikuwa na viongozi na uchaguzi ulikuwa bado haujafanyika.
“Ninawaomba Wanayanga leo (jana) wasifanye makosa, wachague viongozi wazuri ambao watatuendeshea vizuri klabu kwa miaka minne ijayo.
“Nakumbuka kipindi cha mchakato wa uchaguzi huu ilifika wakati ninapigiwa simu na watu ambao walikuwa wanatoa lugha kali wakiwa wanaulizia juu ya uchaguzi huu, sasa hii ni nafasi kwenu, msifanye makosa,” alisema Mkuchika.