SERIKALI mkoani Kilimanjaro imefungua kituo cha kuuza madini ili kudhibiti utoroshaji wa madini yaliyogundulika katika Wilaya za Same, Mwanga, Rombo na Siha.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, aliyasema hayo jana, alipokuwa akizungumza mjini hapa.
“Serikali imeanzisha kituo cha kuuzia madini katika Wilaya ya Same, ambayo inaongoza kuwa na madini mengi zaidi na kuanzishwa kwa kituo hicho, kutaisaidia Serikali kukusanya mapato sahihi yatokanayo na madini pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini.
“Serikali kupitia wataalamu kutoka ofisi ya madini, wamebaini uwepo wa madini mengi katika Wilaya za Same, Mwanga, Rombo na Siha.
“Kwa kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kutorosha madini, kuanzishwa kwa kituo hicho katika wilaya hiyo kutasaidia kudhibiti utoroshaji wa madini katika wilaya hizo.
“Pamoja na hayo, katika tafiti zilizofanywa na timu ya wataalamu karibu wilaya zetu zote zina madini, hivyo mkoa umeona umuhimu wa kuanzisha kituo ndani ya Wilaya ya Same kwanza kutokana na kuongoza kuwa na aina nyingi za madini,” alisema Mghwira.
Kwa mujibu wa Mghwira, lengo la Serikali kuanzisha vituo hivyo vya kuuzia madini ni kutaka kujua uzalishaji wa madini katika eneo husika na kuwatambua wachimbaji wenye leseni na wasio na leseni.
Wakati huo huo, mkuu huyo wa mkoa alisema baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi katika Wilaya ya Same yaligundulika kuwa na madini aina ya kopa, vito, rubi, dhahabu na mengineyo.
Naye Mkuu wa Wilaya Same, Rosemary Sinyamule, alisema kuanzishwa kwa kituo hicho wilayani Same ni fursa kwa wachimbaji wa madini na kwamba watapata soko la uhakika na kwa bei halali kwa mujibu wa sheria.