Licha ya Kushindwa Mabingwa hao wa Tanzania Walionyesha Mchezo wa Kiwango cha juu



Mabingwa wa soka Tanzania, Simba almanusura iandike Historia kwa kuitandika Sevilla ya Hispania iliyosheheni nyota wake kibao.

Katika mchezo wa kirafiki uliovuta hisia za mashabiki wengi Afrika Mashariki, Simba imelala kwenye uwanja wa nyumbani jijini Dar es Salaam kwa kufungwa mabao 5-4 dhidi ya Sevilla.

John Bocco, nahodha wa Simba aliitanguliza timu yake kwa bao la mapema la dakika 8 kabla ya Mieddie Kagere kuongeza la pili dakika ya 15 kutokana na makosa ya beki wa Sevilla.

Sergio Escudero alifungua kalamu ya mabao kwa Sevilla kwa bao la dk ya 24 kabla ya Bocco tena kuipeleka Simba mapumziko ikiwa na ushindi wa mabao 3-1.

Kipindi cha pili Simba iliendelea kushambulia kwa kasi, ikiacha Sevilla ikimiliki mpira kabla ya kumsahau mkongwe Nolito kupunguza uongozi wa Simba kwa bao lake la dakika ya 49.

Kuingia kwa bao hilo kuliongeza hamasa ya wachezaji wa Sevilla walioongozwa na nyota wake Wissam ben Yeder, Ever Banega, Aleix Vidal, Jesus Navas na Sergio Escudero.

Licha ya Clatous Chama kuongeza bao la nne kwa Simba, mabao matatu ya lala salama ya Promes, Munir na Nolito yakazima ndoto za Simba za kusheherehesha ubingwa wao wa ligi kuu ya Tanzania, walioutwaa Jumanne wiki hii.

Pamoja na kufungwa mabao 5-4, Simba imedhihirisha mabadiliko makubwa kwa kuonyesha kiwango bora karibu muda wote wa mchezo.

Umiliki wa Mpira vs Mabao

Mpaka kipindi cha kwanza kinakamilika, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 3-1. Sevilla ikimiliki mpira kwa asilimia 54 dhidi ya 46 ya Simba, lakini Simba ilionekana hatari zaidi golini kwa Sevilla, na ilitengeneza nafasi kama 6 katika kipindi hicho cha kwanza ikiwemo ya mwanzoni kabisa mwa mchezo, ambapo Mzambia Cloutus Chama, alipoteza akiwa umbali wa mita mbili tu golini.

Kwa namna ilivyocheza, Simba inastahili pongezi kubwa kwa kuweza kupata angalau magoli 4 langoni mwa Sevilla, ambayo ni miongoni mwa timu iliyoruhusu mabao machache kwenye ligi ya Hispania (La liga), ikiruhusu mabao 47 tu msimu huu, ikishika nafasi ya 9.

Barcelona yenye washambuliaji wakali duniani wakiongozwa na Lionel Messi na Luis Suarez, ukiacha ushindi wa 6-1 iliyoupata dhidi ya Sevilla mwezi Januari kwenye kombe la Mfalme (Copa del Rey).

Katika mechi sita zilizopita, imepata ushindi kwa tofauti ndogo ya bao moja ama mawili dhidi ya Sevilla.

Hii ni kuonyesha kwamba washambuliaji wa Simba, wamefanya kazi kubwa kupata mabao hayo manne kwenye mchezo huo, ambayo watayakumbuka katika maisha yao.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad