Maamuzi ya Serikali baada ya Wakurugenzi kuzuiwa kusimamia Uchaguzi


SERIKALI imewasilisha notisi katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuhusu kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Bob Wangwe dhidi ya mwanasheria mkuu wa Serikali (AG) na wenzake.

Uamuzi huo wa Serikali umebainishwa jana Jumatatu, Mei 13, 2019 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Aderladus Kilangi, wakati akizungumza na wanahabari kutoa msimamo wa Serikali kuhusu hukumu hiyo ya Mahakama Kuu.

Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu, Dk. Atuganile Ngwala, Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo ilibatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Pia ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Katika hukumu hiyo mahakama hiyo ilisema kwamba vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi ikibainisha kuwa wakurugenzi hao huteuliwa na Rais aliyeko madarakani ambaye hutokana na chama tawala na kwamba wengine ni wanachama wa chama cha mamlaka inayowateua jambo ambalo huathiri utendaji wao katika kutenda haki.

Pia ilisema kwamba sheria haijaweka ulinzi kwa NEC kumteua mtumishi yeyote wa umma kuhakikisha kuwa anakuwa huru katika kutekeleza majukumu yake..
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad