Mganda huyo hivi karibuni aliwaaga mashabiki wa timu hiyo kwa kupitia mtandao wa kijamii kwa kuweka picha yake na ujumbe wa kuaga ambao ulizua mjadala mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, Okwi anataka dau kubwa zaidi ya msimu uliopita la kusajiliwa ambalo ni Shilingi Milioni 115 alilosajiliwa pia Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, kama mshambuliaji huyo akiendelea na kung’angania dau hilo, basi hawataendelea nae msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa na badala yake watamsajili mwingine mbadala wake mwenye uwezo zaidi yake.
“Kikosi chetu cha msimu ujao kinatarajiwa kuwa mabadiliko makubwa kwa kusajili wachezaji wenye uwezo na uzoefu wa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika tutakayoshiriki, mwakani na kubwa zaidi kulichukua taji hilo. “Hivyo, tulichopanga ni kusajili wachezaji waliowahi kuzipa mafanikio timu zao kupitia michuano mikubwa Afrika, hivyo kwa gharama yoyote tutakuwa tayari kumsajili mchezaji kutoka nje ya nchi.
“Hivyo, huyo Okwi kama anataka kuondoka milango ipo wazi, kama uongozi haupo tayari kutoa dau hilo la usajili analolitaka kutokana na kiwango chake alichonacho hivi sasa katika kuelekea michuano mikubwa Afrika,”alisema mtoa taarifa huyo licha ya kutotaka kutaja dau lenyewe.
Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji (C.E.O) wa klabu ya Simba kuzungumzia hilo alisema kuwa “Hilo suala litajulikana hivi karibuni kwani tayari uongozi umeshaanza kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji watakaongeza mikataba yao na kati ya hao yupo huyo Okwi tusubirie kila kitu kitajulikana.”