Serikali imesaini mkataba wa awali na kampuni sita ya kununua korosho kati ya zilizoomba kununua korosho hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 16, 2019 Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema baada ya Kampuni ya Indo Power ya nchini Kenya kushindwa kununua korosho wameendelea kusaini mikataba ya awali.
“Tumeendelea kusaini mikataba mingine na makampuni mengine, mikataba ambayo tumeisaini ni ya awali.
“Mpaka sasa tumesaini na makampuni sita nisingependa kuyataja kwa majina kwa sababu tunajua hali halisi ya makampuni ya korosho watu wanafuatiliana, wanaharibiana biashara pamoja na majina.
“Lakini kuna kampuni moja tuliikaribisha wiki iliyopita imekuja kukagua maghala ya korosho wamejiridhisha kwamba korosho yetu ni safi na haijaharibika na tumepeleka kwenda kuhakiki TBS na wameenda kufanya uhakiki katika nchi yao na wamejihakikishia kwamba ni nzuri na wanajiandaa kulipa.
“Hawa mabwana wakilipa tunawakabidhi korosho mara moja,”alisema Waziri Kakunda.
Akitoa ripoti ya maagizo aliyoagizwa na Rais Dk. John Magufuli wakati akiapishwa, Novemba 12 mwaka jana ya kusimamia ununuzi wa korosho, Kakunda alisema tangu Novemba 13 mwaka jana hadi Mei 15 mwaka huu zimeweza kukusanywa tani 225,000.
“Kati ya hizo tani 2,200 zinaendelea kubanguliwa na viwanda vya ndani kwa mikataba maalum. Maana yake zinabaki tani 228,000 katika maghala."Alisema