Katibu tawala Wilaya ya Mbozi, Tusubilege Benjamin amesema Sh15.2milioni za mauzo ya vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo 760 katika halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, hazijulikani zilipo.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi Alhamisi Mei 30, 2019 katika kikao cha watendaji wa vijiji, kata, wakuu wa idara za halmashauri na madiwani.
Amesema Wilaya ya Mbozi ilikabidhiwa vitambulisho 15,480 na waliopewa kwa ajili ya kuwapatia wafanyabiashara wadogo ni watendaji na baadhi yao wameshindwa kuwasilisha fedha ama vitambulisho hivyo.
Benjamin amewaonya watendaji walioshindwa kuwasilisha vitambulisho hivyo ama fedha kuwa wanahatarisha ajira yao.
Mara ya kwanza Rais Magufuli alitoa vitambulisho 670,000 kuwatambua wafanyabiashara wadogo nchini Tanzania kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa.
ilikuwa Jumatatu Desemba 10, 2018 kwenye mkutano wake na watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakuu wa mikoa yote nchini humo kujadili namna ya kuboresha mazingira ya ukusanyaji mapato.
Amesema kwa muda mrefu amekuwa akiiagiza TRA pamoja na halmashauri kutowatoza kodi wajasiriamali wadogo ambao mitaji yao haizidi Sh4 milioni lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.
Kila Mkoa ulipewa vitambulisho 25,000 na kila mjasiriamali mdogo alilipia Sh20,000 na fedha hiyo kupelekwa TRA.
Kwa malipo hayo, kila mkuu wa Mkoa alipaswa kukusanya Sh500 milioni na ikilazimu aagize vitambulisho vingine kwa ajili ya watakaovihitaji.
Siku hiyo kiongozi mkuu huyo wa nchi alisema hajaridhishwa na utaratibu wa kuunganisha kitambulisho cha TRA na kile cha Taifa kuwatambua wafanyabiashara wadogo akibainisha baadhi yao hutozwa kodi nje ya maagizo.
Baada ya miezi kadhaa baadhi ya Mikoa iliongezewa idadi ya vitambulisho hivyo.
Mbozi: Milioni 15.2 za Mauzo ya Vitambulisho vya Wamachinga Hazionekani
0
May 31, 2019
Tags