Mshambuliaji nyota wa mabingwa wa ligi ya Ubelgiji klabu ya Genk na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Samatta huenda akatua Ligi Kuu ya England (Primia) msimu ujao.
Samatta maarufu kama Samagoal, amedokeza kuwa kuna vilabu sita vya Ligi ya Primia ambavyo vinapigana vikumbo kumsajili nyota huyo.
"Kwa sasa sipo katika nafasi nzuri ya kuelezea ni klabu gani lakini pia kuna klabu nyingine mbili kutoka Hispania ambazo zimekuwa zikiisaka saini yangu. Hata hivyo, mimi ndoto zangu ni kucheza katika Ligi Kuu ya England," Samatta ameliambia gazeti la Mwananchi.
Hii si mara ya kwanza kwa Samatta kuhusishwa na uhamisho wa kwenda Ligi ya Premia, lakini inaonekana kuwa safari hii mambo yameiva.
"Ndiyo, nitaondoka mwishoni mwa msimu huu...(klabu ya England) moja inanifukuzia sana na imekuwa ikipiga simu kwa wakala wangu kila siku," amesema Samatta.
Katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari mwaka huu, klabu ya Cardiff ilituma ofa ya Pauni milioni 13 kumng'oa Genk, lakini uhamisho huo ukakwama.