KATIKA toleo la jana la Gazeti la Spoti Xtra, mshambuliaji Ibrahim Ajibu wa Yanga alinukuliwa akisema hivi: “Kwangu mimi mpira ni kazi yangu, timu ambayo inanifuata ikafuata utaratibu nitaenda, sina tatizo lolote…”
Kauli hiyo aliitoa baada ya kuulizwa juu ya uhamisho wake kwenda Simba, sasa Gazeti la Championi Ijumaa limefahamishwa kuwa staa huyo ameshafikia hatua nzuri ya dili lake hilo na yupo njiani kurejea Simba kwa dau la shilingi milioni 85.
Taarifa hizo zimekuja ikiwa ni siku chache tangu zivuje taarifa za kiungo huyo kurejea Msimbazi kutokana na mkataba wake wa miaka miwili ndani ya Yanga kumalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi. Kwa mujibu wa kanuni za soka za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuhusu usajili, mchezaji anaruhusiwa kusaini mkataba wa awali na klabu nyingine ikiwa muda wa mkataba wake wa klabu anayoichezea ukiwa umebaki miezi sita au chini ya hapo.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ambazo zimefika mezani mwa gazeti hili ni kuwa kiungo huyo amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba kwa dau hilo alilowekewa mezani. Mtoa taarifa huyo alisema, kiungo huyo amesajiliwa na Simba kutokana na ushawishi mkubwa kutoka kwa mwekezaji na bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo’ ambaye anavutiwa na kiwango cha nyota huyo.
“Ajibu ni kweli amesaini Simba lakini upo usiri mkubwa kati ya mchezaji na viongozi wa Simba, kama unavyofahamu yeye bado ana mkataba na Yanga unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. “Dau lake lilifanywa siri, lakini hivi sasa limeanza kujulikana ambalo ni shilingi milioni 85 ambazo zilimshawishi yeye akubali kusaini mkataba wa miaka miwili.
“Pia, kiungo huyo atakuwa anapokea mshahara wa shilingi milioni tano kwa mwezi kwa kipindi chote atakachokuwepo Simba kwa muda wa miaka miwili,” alisema mtoa taarifa. Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Simba, Anold Kashembe juu ya taarifa hizo alisema;
“Muda wa usajili bado ni vema tukasubiri ufike muda, hivi sasa viongozi akili zetu zote tumezihamishia kwenye michezo tuliyoibakisha ya ligi na kikubwa ni kuchukua ubingwa. “Kingine, hata kama ningethibitisha kuwa amesaini mkataba, basi nisingeweka wazi dau la usajili, kwani hilo suala ni nyeti ni siri kati ya mchezaji na viongozi,” alisema Kashembe.