Akizungumza na waandishi wa habari jana Mei 3, jijini Dar es Salaam, Mratibu wa mtandao huo kitaifa, Onesmo Olengurumwa, amesema wamesikitishwa na taarifa za kutoweka kwa wakili huyo huku wakiviomba vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa haraka ili apatikane.
Amesema taarifa za kutoweka kwa Mbunda, ambaye pia ni Mwanasheria wa Hifadhi ya Wanyama Arusha, zilitolewa Aprili 28 mwaka huu zinashangaza wengi na kuomba suala hilo lichukuliwe kwa uzito ili wakili huyo apatikane.
Olengurumwa amesema kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa rafiki wa karibu wa Wakili huyo, magari yaliyotumika kumkamatia hayakuwa na namba za gari na alikamatwa eneo la USA River jijini Arusha, na hajulikani alipo hadi sasa.
“Matukio ya kupotea kwa watu na mawakili na watetezi wengine wa haki za binadamu yamekuwa yakiongezeka hapa nchini na hakuna jitihada zozote zinazochukuliwa na hata kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Ikumbukwe kwamba ni takribani miaka minne sasa tangu wakili wa kujitegemea, Philibert Gwagilo, alipopotea na hadi sasa hajulikani alipo, matukio haya ya kupotea kwa watu yanapojitokeza ni lazima hatua za haraka za kiuchunguzi zichukuliwe ili kusaidia upatikanaji wake,” amesema.
Naye dada wa Wakili Mbunda, aliyejitambulisha kwa jina la Upendo, huku akibubujikwa na machozi amesema kaka yake alipotea tangu Aprili 28 mwaka huu, ma kwa mujibu wa maelezo ya rafiki yake aliyekuja kutoa taarifa nyumbani kwao alidai kuwa alikamatwa na watu waliojitambulisha kuwa ni maaskari.
Upendo amesema tangu tarehe hiyo mpaka leo kaka yake hajaonekana wala hawajafanikiwa kumpata katika kituo chochote cha polisi hapa nchini jambo ambalo anadai limewashtua na linaendelea kuwatia hofu kwakuwa hawana baba wala mama na walikuwa wakimtegemea yeye katika familia yao.
Hata hivyo namba ya Kamanda Polisi, Mkoa wa Arusha, ilipopigwa ili kuelezea tukio hilo kama wanalifahamu simu ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wake na kusema atamuelezea mkuu wake kuhusu suala hilo.