Mwongozo Watolewa Kwa Wakaguzi Katazo Matumizi Mifuko ya Plastiki



Dar es Salaam. Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),  Joseph Malongo ametoa mwongozo kwa wakaguzi na watekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki katika halmashauri zote nchini Tanzania.

Katazo la matumizi ya plastiki litaanza kutumika Juni Mosi, 2019  baada ya Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa kutangaza Aprili 9, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya ofisi yake.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana Mei 23, 2019,  Malongo amesema ukaguzi utafanyika madukani, magengeni, sokoni, maduka makubwa, kwenye maghala, mipakani, viwandani na katika maeneo mengine yanauzwa bidhaa.

Amesema wakati wote wajitambulishe na kuonyesha vitambulisho vyao kwa wahusika kwenye maeneo wanayoyakagua na haitaruhusiwa kumsimamisha na kumpekua mizigo yake ili kutafuta mifuko ya plastiki.

"Hairuhusiwi kuingia kwenye makazi ya watu au kusimamisha magari au vyombo vingine vya usafiri kutafuta mifuko ya plastiki.”

"Iwapo magari au vyombo vya usafiri vitasimamishwa kwa sababu nyinginezo na kukutwa shehena ya mifuko ya plastiki adhabu stahiki itatolewa kwa mujibu wa sheria na wahusika wataelekeza mahala mahsusi itakapopelekwa shehena hiyo," amesema Malongo.

Malongo amesema atakayekutwa  na kosa la kuendelea, kuhifadhi au kutumia mifuko hiyo ataelekezwa kwa kuipeleka na atapigwa faini, endapo akishindwa kuilipa kwa muda aliopewa atafunguliwa mashtaka.

Katika taarifa hiyo, Malongo amesisitiza watakaotozwa na kulipa faini watapewa stakabadhi za Serikali kwa malipo hayo, huku akitaka busara itumike katika utekelezaji wa katazo hilo na matumizi ya nguvu, ikiwemo kuwapiga au kuwabeba na kuwaweka ndani watu hayaruhusiwi.

By Bakari Kiango, Mwananchi 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad