Mzee Mengi Ameondoka Kibabe Sana....

Kwa familia ya mzee wetu, Reginald Mengi, inauma sana kumpoteza mtu waliyempenda. Thamani ya uhusika wake kwao ni kitu kitawatesa mno.

Kwa marafiki na jamaa wa karibu, ni haki kuumia. Ile kampani yake haitakuwepo tena. Kwa namna kubwa, pengo la mzee Mengi haliwezi kuzibika.


Kwa jamii ya Tanzania; japo ni pigo lakini hakuna sababu ya kulia mzee Mengi kufa. Sanasana kuna mambo mawili ya kuchukua kwa kifo chake. Mosi, kusherehekea. Pili, elimu.


Mosi, ile tafsiri ya kumaliza mwendo na kupigana vita vilivyo vizuri, nimeiona kwa Mengi. Miaka 75 ya kuishi. Miaka makumi manne ya mapinduzi ya kiuchumi.


Mengi alitengeneza mabilioni ya fedha wakati wa Tanzania ya Nyerere. Acha Tanzania rahisi ya Mwinyi, Mkapa na Jakaya. Alipigana vita vya kiuchumi na amekufa akiwa mshindi.


Kwa miongo minne, Mengi amekuwa nembo ya Mtanzania mwenye ukwasi. Amewekeza Tanzania. Ameajiri maelfu ya Watanzania. Amehudumia Watanzania. Amewafaa sana Watanzania. Amesaidia Watanzania. Maskini, wajane na vijana Tanzania. Miaka 75, nini alibakisha? Tusherehekee. Amekufa akiwa mshindi.


Pili, elimu ya maisha inapatikana ndani ya kifo cha Mengi. Mzee amekufa kibabe sana. Amekufa akiwa na kila kitu kwenye maisha. Fedha, umaarufu, mke mzuri na watoto. Na amewaacha vizuri. Watafaidi wao na wajukuu zao.


Namna hii mzee Mengi alivyokufa kibabe, inatufundisha kujaa hasira ya kutafuta. Nasi tuje kufa kibabe. Tuwaachie watoto wetu rasilimali za kutosha. Mungu ndiye mpangaji wa kila kitu.


Ni kweli mchango wake ulikuwa bado unahitajika. Na alikuwa na kiu ya kuendelea kutoa huduma kwa nchi kupitia biashara zake. Hata hivyo, tuwe na shukurani. Makumi saba na nusu si haba.


Pole kwa familia. Taifa tusherehekee maisha ya mzee wetu. Ameshinda sana. Ametuhamasisha kufa kibabe. Tutasimulia wajukuu zetu kuhusu shujaa Mengi.


Go well champion.


Ndimi Luqman MALOTO 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad