Marufuku hiyo imekuja kufuatia taarifa za kuwepo kwa baadhi ya Maafisa Wanyamapori ambao wamekuwa wakiwaruhusu Wachimbaji hao kuingia ndani ya Pori hilo nyakati za usiku kwa ajili ya kuchimba mchanga unaodaiwa kuwa una madini kwa makubaliano yaliyo nje ya utaratibu.
Akizungumza na Watumishi wa geti la Doroto katika Pori hilo wilayani Manyoni mkoani Singida, Mhe.Kanyasu amesema kuwa tuhuma hizo za rushwa zitaisha tu pale watakapoimarisha ulinzi katika eneo hilo na sio kukamata vifurushi vya mchanga kwenye geti hilo.
Ameuagiza Uongozi huo kuhakikisha unakamata vifurushi wanavyohisi ndani yake kuna madini na lazima Afisa Madini awepo ili kuhakikisha anataja thamani ya madini pamoja na taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili kukidhi matakwa ya sheria ya utaifishaji wa mali iliyokamatwa.
Baadhi ya Wachimbaji wadogo walionyang'anywa mchanga wao wamedai kwamba Maafisa hao wamekuwa wakikagua magari kwenye geti la kutokea la Doroto na pale wanapokamata vifurushi hivyo bila kujua mchanga huo una madini kiasi gani wamekuwa wakimruhusu mtuhumiwa aende zake bila kumueleza taratibu zozote zile jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Amesema kitendo hicho ni unyang'anyi na uonevu wa hali ya juu na ni kinyume cha sheria kwa sababu sheria ya utaifishaji wa mali iliyokamatwa inampa nafasi mtuhumiwa kujua thamani ya mali aliyokamatwa nayo na ndipo taratibu za kesi kwenda mahakamani hufuata.
Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewaonya Maafisa Wanyamapori katika pori hilo kuacha tabia ya kuwaonesha wachimbaji hao mahali wanapohisi kuwa kuna madini kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Amesema ni ngumu kwa Mwananchi yeyote kujua sehemu ambako kuna madini ndani ya Pori bila kudokezwa na wenyeji ambao ni Wahifadhi wa Pori hilo
Amesisitiza kuwa endapo uchimbaji huo wa madini ndani ya Hifadhi utaendelea kufanyika itakuwa ni ushahidi tosha kuwa Meneja wa Pori hilo kashindwa kazi.
Aidha, Mhe.Kanyasu amewataka kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya Pori hilo ili kukomesha ujangili wanyamapori pamoja na ukataji miti ndani ya Pori hilo.
Kwa upande wake, Meneja wa Pori la Akiba la Rungwa, Patrick Kutondolana amekiri kuwa wamekuwa wakikamata mchanga huo kwa mashirikiano kati ya Kamati ya Ulinzi wa Wilaya hiyo ili kukomesha tabia hiyo ya uchimbaji mchanga ndani ya Hifadhi.
Amesisitiza kuwa si kweli kuwa wamekuwa na ushirikiano na Wachimbaji hao kwa makubaliano ya kupata rushwa ni kwamba hiyo imekuwa njama ya kutaka kuwachafua kwa lengo la kuwakatisha nia.