Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amedai kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu ambao walikuwa na muonekano usioridhisha huku mwenyewe akieleza akiwa na imani kubwa ya kuja kutimiza ndoto zake baadaye.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa jina maarufu 'Baba Keagan', Paul Makonda amechapisha picha ambayo inamuonesha kiongozi huyo akiwa kwenye moja ya meli jijini Mwanza na kuwahasa watu wanaomfuatilia kutokata tamaa.
"Picha hii inanikumbusha safari yangu na mapambano niliyoyapitia, kwa kifupi muonekano huu ni tofauti sana na hali na ndoto niliyokuwa nayo ndani yangu, kwa muonekano wa nje nimedhoofika, nimechoka, mavazi hayaeleweki, uso hauna tumaini na zaidi ya yote siwezi hata kumwaminisha mtu kuwa siku moja nitatimiza ndoto zangu", ameandika Makonda.
"Muonekano huu unawakilisha idadi kubwa ya maisha ya vijana wa kitanzania, ila ndoto yangu ilikuwa tofauti na muonekano huo wa nje, kwani ndani yangu nilikuwa na ndoto inayonisukuma kwenda mbele pamoja na upendo mkubwa wa Mungu" ameendelea kuandika Makonda.
Hivi karibuni, Mkuu huyo wa Mkoa amekuwa akiandamwa baada ya kutoa kauli iliyoleta mkanganyiko hasa kwa watu wa Kilimanjaro kwenye shughuli ya kuaga mwili wa Dr. Reginald Mengi jijini Dar es salaam. Hata hivyo aliomba msamaha kufuatia kauli hiyo.