Rais Magufuli Afanya Mazungumzo Na Rais Wa Afrika Kusini Ikulu Ya Pretoria


Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumapili Mei 26, 2019, amekutana na kufanya mazungujza na Rais  Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Ikulu Jijini Pretoria.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amempongeza Rais huyo kwa kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Afrika Kusini na amemhakikishia kuwa Tanzania itadumisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu na kihistoria na nchi hiyo.

 Rais Magufuli amaesema uhusiano wa Tanzania na nchi hiyo uliasisiwa na Baba wa Taifa wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Nelson Mandela kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ANC (African National Congress).

Amemwambia kuwa ni matarajio yake kuona uhusiano huo unaimarishwa zaidi katika nyanja za uchumi na kukuza lugha ya  Kiswahili.

Rais huyo wa Tanzania, amemshukuru Ramaphosa kwa kumkaribisha na kufanya naye mazungumzo ya siku moja baada ya kuapishwa kwake.

Kwa upande wake, Rais Ramaphosa naye amemshukuru Magufuli kwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake na amemhakikishia kuwa Afrika Kusini inatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika ukombozi wa Taifa hilo.

Hivyo, amemuahidi katika kipindi chake cha uongozi atauendeleza na kukuza zaidi uhusiano huo.

Rais Ramaphosa amesema kufuatia uamuzi wa Afrika Kusini kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili, nchi yake itachukua walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania ili watumike kufundisha somo hilo katika shule za msingi na sekondari.

Aidha, ameahidi kufanya ziara rasmi ya Tanzania kabla ya Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), uliopangwa kufanyika Agosti 2019 nchini Tanzania. Pia, atahudhuria mkutano huo.

Kabla ya mazungumzo hayo,  Rais Magufuli ambaye ameongozana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alimkabidhi Ramaphosa zawadi ya vitabu vya kusoma na kufundishia lugha ya Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Marais hao wawili wamefanya  mazungumzo hayo ikiwa ni kabla ya  Rais Ramaphosa hajatangaza Baraza lake la Mawaziri.

Kesho, Rais Magufuli ataondoka Afrika Kusini kuelekea nchini Namibia ambako atafanya ziara rasmi ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais wa Namibia, Hage Geingob.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad