Rais Magufuli Apokea Gawio TTCL Atoa Agizo Hili kwa Mawaziri

RAIS  John Magufuli leo Jumanne, Mei 21, 2019 ametembelea makao makuu ya Shirika la Mawasiliano la Tanzania (TTCL) na kupokea gawio la Shilingi bilioni 2.1 kwa mara ya pili mfululizo ambalo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na mwaka jana. Gawio hilo limepatikana kutokana na ongezeko la mapato kutoka Sh 119 bilioni mwaka jana hadi Sh 167 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Shilingi milioni 600 milioni.



Akizungumza na wafanyakazi wa TTCL, Magufuli amesema: “Tangu Shirikia la TTCL lianze kuendeshwa na wabia wetu, halikuwahi kutoa gawio hata la shilingi tano kwa miaka 15 na lilikuwa likipata hasara ya Tsh bil.15 kwa mwaka, lakini tangu tulirudishe kwenye mikono ya serikali, shirika hili sasa limeanza kutengeneza faida kubwa.



“Niseme kwa uwazi, TTCL mmekuwa mkipigwa vita sana, vita zingine sio za uwazi ni vita vya chinichini, hata leo kuja hapa kulikuwa na mbinu za kijanja-kijanja kunizuia nisije kupokea gawio, na zimechezwa kwelikweli, hii inathibitisha kuwa nyinyi mnastahili,  lazima tuwasaidie.



“Waziri amesema Mfuko wa Mawasiliano upo chini ya wizara yake, pesa zinachangwa na Watanzania na TTCL ni ya Watanzania, kwa nini inakodi minara ya mashirika mengine na kulipia Sh mil. 700 hadi mil. 800?   Kwa nini usitumie pesa hizo kujenga minara ukawapa TTCL moja kwa moja?



“Mashirika mengine yanalipia kodi, lakini TTCL wanalipa kodi na wanalipa gawio, kwa hiyo faida itayakopatikana itakuwa ni ya serikali, hakuna haja ya kuwaacha TTCL wakateseka, huwezi kumuacha mwanao anateseka na chakula unawapa watu wengine,  lazima tuisaidie TTCL.





“Naomba niletewe orodha ya viongozi ambao wanatumia laini za TTCL na sio ziwepo tu bila kutumika, huwezi kulipwa mshahara wa Serikali na hutumii mtandao huo, asije akawa anaandika meseji tu halafu anaicha, nataka ziwe zinatumika, sijamaanisha msitumie mitandao mingine. Msajili wa Hazina hakikisha ifikapo mwezi Julai, mashirika yote 253 nchini ambayo yamekuwa hayatoi gawio kwa serikali, yawe yametoa gawio la sivyo yafungwe.



“Taasisi zilizojiunga kutumia TTCL, ofisi yangu ya rais haikutajwa, chama changu CCM hakikutajwa, inaonekana hawa hata kwenye ofisi yangu wamo. Kama wananisikia ninataka ndani ya mwezi mmoja tuanze kutumia simu za TTCL na wizara nyingine,” amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad